1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Pengo la digitali latanuka Afrika Mashariki

Mohamed Dahman23 Aprili 2007

Pengo la digitali kati ya maeneo ya mijini na vijijini Afrika Mashariki na kati ya matajiri na maskini linaendelea kutanuka na kuonyesha haja ya kuanzisha juhudi ambazo zitawezesha kila mtu kufaidika kutokana na teknolojia za habari na mawasiliano.

https://p.dw.com/p/CHl9

John Waweru mkurugenzi mkuu wa Tume ya Mawasiliano ya Kenya anasema hata kama wanajibu changamoto zinazoletwa na mapinduzi ya teknolojia ya habari na mawasiliano ni vyema kuwa wenye hisia kwa taathira za tafauti lukuki kati ya matajiri na maskini na kati ya watu wa mijini na vijijini.

Waweru alieleza hayo mapema mwezi huu katika mkutano uliofanyika chini ya usimamizi wa Mashirika ya Waratibu wa Simu na Posta ya Afrika Mashariki mjini Nairobi Kenya.Mkutano huo ulikuwa ni hatua ya kwanza kuelekea kuoanisha sera za teknolojia ya habari na mawasiliano ICT katika eneo hilo li kuhakikisha kukuwa kwa matumizi ya teknolojia mpya.

Ni asilimia tano tu yaani watu milioni saba kati ya milioni 34 nchini Kenya wana miliki simu zile zinazotumia nyaya na za mkono na wengi wa watumiaji hao wako katika miji mikubwa na midogo.

Kwa mujibu wa mkurugenzi mkuu wa Mamlaka Inayosimamia Mawasiliano nchini Tanzania John Nkoma hali hiyo inalingana na nchi yake ambapo watu milioni saba kati ya milioni 34 wa nchi hiyo wana simu za nyaya na zile za mkono na kwa mara nyengine wengi wao wako katika maeneo ya miji.

Katika mahojiano na IPS Nkoma amesema jambo la kutia moyo zaidi ni kwamba kama miaka miaka mitatu iliopita idadi ya watumiaji wa simu hizo ilikuwa ni milioni mbili tu.

Uchunguzi kama huo uliofanywa na Benki ya Dunia umedokeza kwamba zaidi ya asilimia 50 ya huduma za teknolojia ya habari na mawasiliano ICT barani Afrika zimejikita katika maeneo ya mijini juu ya kwamba miji ni maskani ya pungufu ya asilimia 30 ya watu wa bara hilo.

Uganda inaeleza jinsi mambo hayo yanavyoweza kutekelezwa tafauti kabisa.

Mfuko wa teknolojia ya habari na mawasiliano ulioanzishwa miaka minne iliopita nchini humo umesaidia kuanzisha mikahawa ya mtandao na simu,posta na huduma za matarishi katika maeneo ya vijijini.Mfuko huo wa Maendeleo ya Mawasliano Vijijini unatowa ruzuku kwa kampuni kuanzisha vituo vya teknolojia ya habari na mawasiliano katika maeneo ya mbali kabisa ili kuhakikisha upatikanaji wa teknolojia ya habari unatanuka kwa kiwango kikubwa.

Mkurugenzi mtendaji wa Tume ya Mawasiliano ya Uganda Patrick Masambu ameliambia shirika la habari la IPS kwamba wanataraji kila shule ya msingi iwe inaweza kuwa na mawasiliano ya mtandao ifikapo mwaka 2010 na kwamba wanaweka huduma za simu za malipo katika kila parokia.

Mfuko huo unahesabiwa kuwa mfano mzuri wa utekelezaji kwa ajili ya kuziwezesha jamii za kimaskini na vijijini barani Afrika kutumia teknolojia za habari na mawasiliano. Mradi kama huo hivi sasa unafikiriwa kuanzishwa nchini Kenya.

Wakati juhudi hizo zikikaribishwa hiyo sio njia pekee ya kuwavutia wawekezaji kwenye mazingira ya vijijini.Kituo cha Utafiti cha Maendeleo cha Kimataifa ambalo ni shirika la kiserikali la Canada linasema ufunguaji wa masoko pia una dhima ya kutimiza katika hilo ambapo ziada ya hayo miundo mbinu ianzishwe kwenda sambamba na juhudi hizo.

Katika suala la miundo mbinu umeme unatajwa kuwa ni muhimu kabisa na katika kuyakifikia maeneo ya vijijini na yale yalioko mbali inapendekezwa pia kutafsiri kwa lugha za kienyeji maelekezo ya matumizi ya teknolojia hizo.