1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Poland: Serikali mpya yenye muda mfupi

Jacek Lepiarz | Iddi Ssessanga
29 Novemba 2023

Serikali ya Poland iliapishwa Jumatatu. Kile kinachoitwa "Baraza la wataalamu" likiongozwa na Waziri Mkuu Mateusz Morawiecki, limejumlisha mawaziri vijana na lina wanawake zaidi. Lakini je, litaongoza kwa muda gani?

https://p.dw.com/p/4Zahz
Poland| Hafla ya kuapishwa kwa serikali mpya.
Rais Andrzej Duda, kushoto, akipeana mkono na waziri mkuu Mateusz Morawiecki, wakati wa hafla ya kuapishwa mjini Warsaw, Poland, Jumatatu Novemba 27, 2023. Picha: Czarek Sokolowski/dpa/picture alliance

Spika mpya wa bunge la Poland, Szymon Holownia, hakumunya maneno yake. Siku ya Jumanne, siku moja tu baada ya Baraza jipya la Mawaziri la Waziri Mkuu Mateusz Morawiecki kuapishwa, alisema, "Ninapenda sarakasi, lakini sipendi programu hiyo kila wakati."

Uamuzi wa Rais Andrzej Duda wa kukipa chama kilichoshindwa uchaguzi fursa ya kwanza kuunda serikali na kuliapisha Baraza lake la Mawaziri, kulingana na Holownia, "hauhusiani kwa vyovyote na viwango vya kistaarabu vya demokrasia, makabidhiano ya madaraka na utamaduni wa kisiasa."

Aliendelea kusema, "Kilichofanyika jana katika ikulu ya rais hakipaswi kamwe kutokea katika Jamhuri ya Poland." Kuapishwa kwa serikali ya Morawiecki, alisema Holownia, ilikuwa "kofi kwa demokrasia."

Sherehe ya kuapishwa kama nyingine yoyote?

Sherehe za kuapishwa katika ikulu ya rais mjini Warsaw Jumatatu alasiri zilifanyika kama nyingine zote tangu kuanguka kwa ukomunisti nchini Poland miaka 34 iliyopita.

Poland | Hafla ya kuapishwa kwa baraza jipya la mawaziri
Rais wa Poland Andrzej Duda akizungumza wakati wa hafla ambako alimuapisha waziri mkuu Mateusz Morawiecki na baraza lake jipya mjini Warsaw, Poland, Jumatatu Novemba 27, 2023.Picha: Czarek Sokolowski/dpa/picture alliance

Kulikuwa na kupeana mikono na tabasamu, na waziri mkuu na mawaziri wake walikula kiapo cha ofisi, ambacho nchini Poland karibu kila wakati huisha kwa maneno "Ee Mungu nisaidie." Kisha rais alimtakia waziri mkuu kila la heri kabla ya sherehe kukamilika kwa "picha ya familia" ya lazima.

Soma pia: Waziri Mkuu wa Poland apewa jukumu la kuunda serikali

Lakini muonekano wa hali ya kawaida ulikuwa unadanganya. Hii haiku sherehe ya uapisho kama nyingine zote. Duda alimteua kuwa waziri mkuu, mtu ambaye chama chake hakina tena wingi bungeni. Hata washirika watiifu wa kichama, kama vile waziri wa zamani anaeshughulikia mali za taifa Jacek Sasin, aliweka nafasi ya Morawiecki kupata uidhinishwaji wa serikali yake sana sana kwa asilimia 10.

Soma pia: Muungano wa upinzani wafanikiwa wingi wa viti Poland

Wakati wa ukweli utakuja, kwa karibu zaidi katika siku 14: Morawiecki lazima apigiwe kura ya imani bungeni ifikapo Desemba 11.

"Sarakasi ya mwisho ya kisiasa," lilifupisha jukwaa la mtandaoni la Onet. "Serikali haina matumaini ya kushinda kura ya imani," kilisema kichwa cha habari katika gazeti la kila siku la Gazeta Wyborcza. Mbunge wa upinzani Michal Szczerba aliitaja kama "kupoteza muda."

Urari wa wazi wa madaraka

Urari wa madaraka katika bunge la Poland uko wazi: Wakati chama cha Sheria na Haki (PiS) ndicho chama kikubwa zaidi bungeni, kilipata viti 194 pekee katika uchaguzi wa Oktoba - ikiwa ni upungufu sana ya viti 231 vinavyohitajika kutawala.

Morawiecki amekuwa akidai mara kwa mara kwamba yuko kwenye mazungumzo na wabunge wenye nia kutoka vyama vingine, lakini hadi sasa hajaweka wazi jina la hata mtu mmoja anayeweza kuasi kutoka chama kingine.

Wiki iliyopita, alivialika rasmi vyama vyote vya upinzani - isipokuwa Muungano wa Kiraia wa Donald Tusk (KO) - kwenye mazungumzo ya muungano. Vyama viwili vya Kikristo vya Third Way, TD, na New Left viliukataa mwaliko wa Morawiecki. Kwa pamoja na Muungano wa Tusk wa Civi Coalition, vyama hivyo vitatu vinaunda muungano unaoelemea Umoja wa Ulaya, wa mrengo wa wastani wa kushoto ambao umejitangaza kuwa tayari kuongoza.

Ingawa chama cha mrengo mkali wa kulia cha Confederation kilikutana na Morawiecki, kilifanya hivyo tu kumuamba hakitaiunga mkono serikali yake.

Sura mpya na mawaziri wanaorejea

Kuna mawaziri watatu pekee wa zamani katika Baraza jipya la Mawaziri la Morawiecki. Waziri wa Ulinzi Mariusz Blaszczak alibakisha wadhifa wake, Waziri wa masuala ya Ulaya Szymon Szynkowski alipandishwa cheo na kuwa waziri wa mambo ya nje na aliyekuwa Waziri wa Kazi Marlena Malag aliteuliwa kuwa waziri wa maendeleo.

Poland | Hafla ya kuapishwa kwa mawaziri wapya
Waziri Mkuu wa Poland Mateusz Morawiecki, kushoto, akiwa na wajumbe wa serikali yake mpya mjini Warsaw, Poland, Jumatatu, Novembe 27, 2023.Picha: Czarek Sokolowski/dpa/picture alliance

Wizara zilizosalia zilikwenda kwa watumishi wakuu wa serikali, ambao wengi wao wamefanya kazi kwa karibu na Morawiecki. Dominika Chorosinska, ambaye aliigiza katika tamthilia kwa miaka mingi, ameteuliwa kuwa waziri wa utamaduni.

Soma pia:Matumaini ya EU baada ya uchaguzi wa Poland 

Wizara tisa kati ya 16 zinaongozwa na wanawake - rekodi katika siasa za Poland. Duda alizungumza juu ya "wakati wa kihistoria" kwa nchi. Watu wengi walioko katika Baraza la Mawaziri wana umri wa miaka 40, na mawaziri wengine ni wachanga zaidi.

Akizungumza kwenye televisheni ya taifa ya Poland, Morawiecki alitoa wito wa kuungwa mkono na kukosoa upinzani kwa kuendeshwa na msukumo wa kulipiza kisasi.

"Inafaa kutafuta kile kinachofungamana badala ya kile kinachotenganisha," alisema, akiongeza kuwa anatumai kungekuwa na "watu waadilifu 231" bungeni kukubali "Dekalojia yake ya masuala ya Poland."

Mabadiliko ya msimamo ya Kaczynski

Katika mahojiano na shirika la habari la serikali PAP siku ya Jumatatu, kiongozi wa PiS Jaroslaw Kaczynski alisema Baraza la Mawaziri la wataalam lilikuwa wazo lake.

"Muhimu ni kwamba kusiwe na wanasiasa wengi katika serikali hii," alisema. "Tunataka kuonyesha kwamba inawezekana kutawala tofauti."

Mwandishi wa habari Jacek Nizinkiewicz aliomba kutofautiana. "Serikali hii imejengwa juu ya uwongo," aliandika katika gazeti la Rzeczpospolita. "Tunapaswa kupata sura mpya na wataalam," alisema. "Badala yake, tunapata majina ya zamani na sio wataalam wowote."

Kaczyński anataka kutumia kikamilifu muda unatolewa na katiba inaruhusu kulainisha njia ya chama chake katika viti vya upinzani. Nyadhifa nono bado zinatolewa kwa wanachama waaminifu wa chama na ruzuku nyingi kwa taasisi zinazoshirikiana na PiS.

Warsaw Poland | Kikao cha kwanza cha Bunge | Donald Tusk
Kiongozi wa Jukwaa la Kiraia, KO, Donald Tusk akihudhuria kikao cha kwanza cha bunge jipya la Poland mjini Warsaw, Novemba 13, 2023.Picha: Kacper Pempel/REUTERS

Serikali imejaribu - hadi mwisho - kujilinda kisheria na kifedha dhidi ya uingiliaji unaowezekana wa serikali ijayo. Mabadiliko ya kanuni yaliyofanywa Jumatatu yalikusudiwa kuimarisha utawala wa PiS juu ya vyombo vya habari vya umma inavyodhibiti.

Soma piaUpinzani nchini Poland wafanya mkutano mkubwa wa kampeni:

Wakati uchaguzi wa serikali za mitaa ukitazamiwa kufanyika mwezi Aprili na uchaguzi wa Bunge la Ulaya mwezi Juni, chama hicho pia kina nia ya kutangaza simulizi ambayo itawaweka wapiga kura wake waaminifu, ambayo ni kwamba PiS ilipigana hadi mwisho mchungu na kwamba upinzani uovu, ambao kinadai unadhibitiwa na Ujerumani, ndiyo wa kulaumiwa kwa ukweli kwamba serikali ya PiS iliyofanikiwa haikuweza kuendelea na kazi yake.

Bunge launda tume za uchunguzi

Licha ya kile ambacho wengi wanakiona kama misheni iliyofeli ya Morawiecki kuunda serikali, muungano wa mrengo wa kushoto tayari unafanya kazi bungeni, ukijiandaa kwa siku ambayo unaweza kuchukua hatamu za serikali.

Utaratibu wa bunge wa utoaji wa ufadhili wa serikali kwa IVF tayari umezinduliwa. Pia kuna mipango ya kuunda tume tatu za uchunguzi siku ya Jumanne. Miongoni mwa masuala mengine, wabunge wanataka kujua ikiwa idara ya ujasusi inayodhibitiwa na serikali ya PiS ilitumia programu ya Pegasus kupeleleza upinzani. Tume nyingine itachunguza madai kwamba visa za Poland zilitolewa kwa hongo ya pesa taslimu barani Afrika na Asia.

Serikali ya baadaye ya Poland yenye nafasi halisi ya kupata wingi wa wabunge, ambayo Donald Tusk ataongoza, pengine haitaapishwa kabla ya Desemba 13. Baadhi ya vyombo vya habari vimedokeza kuwa hicho ni kitendo cha kisasi cha rais. Juu ya yote, kwa Wapoland wengi, Desemba 13 ilikuwa siku ambayo jeshi la kikomunisti liliweka sheria ya kijeshi mnamo 1981.

Donald Tusk achaguliwa tena Rais Baraza la EU

Kwa upande wake, Tusk anaangazia uhusiano mzuri zaidi na tarehe hii, akitangaza, "Hii ndiyo siku ambayo tunaadhimisha Sikukuu ya Mtakatifu Lucy, ambayo inaashiria mwanga katika kina cha baridi kali."