1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Abdullahi Yusuf wa Somalia Ajiuzulu

Eric Kalume Ponda29 Desemba 2008

Rais Abdullahi Yusuf wa Somalia amejiuzulu.Rais Yusuf amejiuzulu hii leo, hatua inayofikisha kikomo utawala wake wa miaka minne.

https://p.dw.com/p/GObl
Rais Abbdullahi Yusuf wa Somalia aliyejiuzulu.Picha: AP


Taifa hilo halijakuwa na amani kwa takriban miongo miwili, tangu kutimuliwa madarakani kwa aliyekuwa kiongozi wa kiimla nchini humo Siad Barre mwaka wa 1990.



Kujiuzulu kwa Rais Yusuf huenda kutadidimiza juhudi za viongozi wa mataifa ya kanda katika kutafuta amani nchini humo, na kulitumbukiza taifa hilo katika hali ngumu zaidi ya kisiasa .


Rais Abdullahi Yusuf aliwasilisha barua yake ya kujiuzulu kwa spika wa bunge la nchi hiyo Sheikh Aden Madobe. Kulingana na maazimio ya mkataba wa utawala kwa serikali hiyo ya mpito, spika huyo wa bunge sasa atachukua usukani wa kuliongoza taifa hilo kwa muda, hadi pale rais mpya atakapochaguliwa.


Akikubali barua hiyo, spika huyo wa bunge alimpongeza Rais Yusuf akitaja hatua hiyo kuwa ya ujasiri na kwa kuzingatia na kudumisha mkataba wa serikali hiyo ya mpito.


Rais Abdulahi Yusuf alisema kuwa amechukua uamuzi huo, kwa kuzingatia ahadi aliyotoa alipokuwa akiingia madarakani kwamba angejiuzulu endapo atashindwa kuleta amani na uthabiti kwa taifa hilo, na kamwe hangetaka kukiuka mkataba huo.


Rais Abdullahi Yusuf alichaguliwa kuliongoza taifa hilo mwaka wa 2004 kufuatia mashauriano ya amani ya muda wa miaka miwili yaliyoleta pamoja makundi hasimu nchini Somalia na kuonmgozwa na viongozi wa mataifa ya Africa Mashariki.


Serikali hiyo na mpito imekabiliwa na changamoto nyingi na migogoro ya ndani tangu kuundwa kwake, hatua iliyopelekea rais huyo kumuachisha kazi waziri wake mkuu Nur Hassan Hussein wiki iliyopita.


Hatua hiyo ilishtumiwa vikali na viongozi wa kanmda hiyo hususan Kenya ambayo imekuwa katika mstari wa mbele kutafuta amani nchini Somalia. Serikali hiyo ilimpiga marufuku Rais Yusuf kuingia nchinin humo kwa kumtaja kuwa kikwazo cha kupatikana kwa amani nchini Somalia.


Waziri mkuu Hussein aliteuliwa mwezi Novemba mwaka wa 2007 na kuchukua mahala pa aliyekuwa mtangulizi wake Ali Mohammed Gedi ambaye pia alilazimishwa kujiuzulu.


Utawala wa Rais Yusuf ulishindwa kukabiliana na ongezeko la ghasia nchini Somalia, hali iliyopelekea kuchupuka kwa makundi mengi ya wapiganaji. Hata hivyo serikali hiyo ya Rais Abdullahi Yusuf imekuwa serikali pekee iliyotambuliwa na jamii ya kimataifa tangu kuangushwa kwa utawala wa Siad Barre mwaka wa 1991.


Rais Yusuf mwenyewe ameilaumu jamii ya kimataifa kwa kushindwa kuisaidia Serikali yake ya mpito katika kanda hiyo ya upembe mwa Africa.


Serikali hiyo imekabiliwa na upinzani mkali ambapo kilele chake ilikuwa mwaka wa 2006,kutoka kwa kundi la wapiganaji wa mahakama za kiislamu waliochukua usimamizi wa eneo kubwa la Kusini na kati mwa nchi hiyo. Hatua hiyo ilipelekea majeshi aya Ethiopia kuingilia kati na kuwatimua wapiganaji hao wa mahakama za kiislamu.

Sasa Rais Yusuf anatarajiwa kuondoka makao makuu ya serikali hiyio mjini Baidoa, na kuelekea jimbo la Puntalnd lililojitangazia uhuru wake. Abdullahi Yusuf amekuwa rais wa jimbo hilo kati ya mwaka wa 1989n na 2004 alipoteuliwa rais wa taifa la Somalia.


Wadadisi wanahoji kuwa hatua hiyo huenda ikachochea mapigano zaidi ya kikabila nchini Somalia na kuongezeka kwa mashambulizi ya makundi ya wanamgambo hasa ikizingatiwa kwamba wafuasi wa kundi la wapiganaji wa mahakama za kiislamu bado wanaendesha shughuli zao katika vitongoji vya mji mkuu wa nchi hiyo.


Yadaiwa kuwa makundi ya wapiganaji nchini humo yanasimamia vitongoji vya mji mkuu wa Mogadishu na eneo la kusini mwa nchi hiyo na huenda wakachukua usimamizi wa taifa zima endapo majeshi ya Ethiopia yataondoka nchini humo.


Zaidi ya wanajeshi 3,000 wa Ethiopia wamekuwa wakidumisha usalama nchini humo kwa muda wa miaka miwili,ingawa wanatarajiwa kundoka mwishoni mwa mwaka huu.