1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroNiger

Rais Bazoum aapa kuilinda demokrasia ya Niger

Sylvia Mwehozi
27 Julai 2023

Rais wa Niger Mohamed Bazoum ameapa kulinda vikali mafanikio ya kidemokrasia "yaliyopatikana kwa bidii" baada ya kushikiliwa na kikosi maalum cha walinzi wa rais ambacho kilitangaza kwamba kimechukua madaraka.

https://p.dw.com/p/4USRT
Rais Mohamed Bazoum
Rais wa Niger Mohamed BazoumPicha: Facebook/Präsidentschaft der Republik Niger

Rais Bazoum alishikiliwa mjini Niamey siku ya Jumatano na wanajeshi wa kikosi maalumu cha ulinzi wa rais ambao baadae walitangaza kwamba wamechukua madaraka. Katikati mwa miito ya kulaani mapinduzi hayo kutoka Jumuiya za kikanda na kimataifa, Rais Bazoum ameonekana kushikilia msimamo wake kwamba yeye bado ni rais wa taifa hilo. Kupitia mtandao wa Twitter ambao hivi sasa unajulikana kama X, aliandika kwamba "maendeleo yaliyopatikana kwa bidii yatalindwa".

Naye waziri wa mambo ya nje wa taifa hilo Hassoumi Massoudou katika mahojiano na kituo cha Runinga cha France 24 alisema kuwa "madaraka ya kisheria na halali" nchini Niger ni yale yanayotekelezwa na rais aliyechaguliwa. Ameeleza kuwa Rais Bazoum "yuko na afya njema" na kwamba kulikuwa na "jaribio la mapinduzi" lakini si "jeshi lote limehusika".

Usiku wa kuamkia leo, viongozi wa mapinduzi walijitokeza kupitia Televisheni na kutangaza kwamba wanasimamisha "taasisi zote" na kuanzisha hatua nyingine ikiwemo kufunga mipaka ya nchi na marufuku ya kutotoka nje usikuhadi pale watakapotoa "taarifa nyingine". Kanali Meja Amadou Abdramane, ambaye ni msemaji wa Kamati ya kitaifa ya wokovu wa watu CNSP akiongozana na wanajeshi wengine 9 waliovalia sare za kijeshi alisema kuwa.

Niger |  Amadou Adramane
Kanali Meja Amadou Adramane msemaji wa kikosi kilichofanya mapinduziPicha: ORTN/REUTERS TV

"Taasisi zote za awamu ya saba ya Jamhuri zimesimamishwa, makatibu wakuu wa wizara watasimamia shughuli za kila siku, vyombo vya ulinzi na usalama vinasimamia hali hiyo, na washirika wote wa nje wanaombwa wasiingilie, " alisema Kanali Meja Amadou Abdramane.

Rais wa nchi jirani ya Benin Patrice Talon alikuwa njiani kuelekea Niamey hii leo (siku ya Alhmis) kwa juhudi za upatanishi, wakati viongozi wa kikanda na kimataifa wakiendelea kutoa wito wa kuachiliwa mara moja kwa rais Bazoum, ambaye aliingia madarakani miaka miwili iliyopita katika makabidhiano ya kwanza ya amani ya madaraka tangu nchi hiyo ipate uhuru kutoka Ufaransa mwaka 1960.

Soma pia: Wanajeshi wa Niger wadai kumuondoa madarakani Rais Bazoum

Naye waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken amesema kuwa amezungumza na Bazoum na kutoa uungwaji mkono wa Washington.

"Nilizungumza na Rais Bazoum mapema asubuhi ya leo na kuweka wazi kwamba Marekani inamuunga mkono kwa dhati kama rais aliyechaguliwa kidemokrasia wa Niger. Tunaomba aachiliwe mara moja. Tunalaani juhudi zozote za kunyakua mamlaka kwa nguvu."

Kitisho kilianzia hapa: Niger yakumbwa na kitisho cha "mapinduzi ya kijeshi"

Wizara ya mambo ya nje ya Ujerumani imesema kuwa inafuatilia kwa ukaribu matukio ya nchini Niger "kwa wasiwasi mkubwa" na kulaani jaribio la kikosi maalum cha walinzi wa rais cha kupindua serikali. Taarifa ya wizara imeongezea kuwa "vurugu sio njia ya "kulazimisha maslahi ya kisiasa au binafsi" na kutaka Rais Bazoum kuachiliwa mara moja.

Vyanzo: AFP, Reuters