1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa Ghana anakwenda Kenya kwa upatanishi.

8 Januari 2008
https://p.dw.com/p/CmRw

Nairobi. Mwenyekiti wa umoja wa Afrika , rais John Kufour wa Ghana , anatarajiwa baadaye leo kuwasili nchini Kenya kwa mazungumzo na rais Mwai Kibaki na kiongozi wa upinzani Raila Odinga. Kibaki anatarajia kuwa rais Kufour atamuunga mkono wakati Odinga anatarajia kuwa ziara hiyo itaanzisha juhudi za kimataifa za upatanishi ili kumaliza ghasia zilizosababishwa na matokeo ya uchaguzi ambapo mamia ya watu wameuwawa na wengine 250,000 kukimbia makaazi yao.

Hata hivyo rais Mwai Kibaki pamoja na kiongozi wa upinzani Raila Odinga wametoa maelezo ya maridhiano ili kumaliza mzozo huo , kwa kutangaza kutofanyika kwa maandamano pamoja na kukubali kuzungumza kutokana na mbinyo wa Marekani.

Mjumbe wa ngazi ya juu wa Marekani anayeshughulikia masuala ya Afrika Jendayi Frazer amesema kuwa hesabu ya kura ambayo ndio chanzo cha mzozo iliendewa kinyume na pande zote mbili zinaweza kuwa zimehusika.

Kuingilia kati kwa Marekani kunaonekana kuwa kunaleta mafanikio katika mzozo huo, kwa kuwa kila upande sasa unapunguza jazba. Viongozi watatu wa zamani wa mataifa ya Afrika pia wamewasili mjini Nairobi. Joachim Chisano wa Msumbiji amesema kuwa watatembelea maeneo ya mabanda ambayo yamekumbwa na machafuko leo Jumanne lakini hakusema iwapo yeye binafsi , rais wa zamani wa Zambia Kenneth Kaunda na Benjamin Mkapa wa Tanzania watashiriki katika upatanishi.