1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapigano yanaendelea kaskazini magharibi mwa Pakistan

Abdu Said Mtullya13 Mei 2009

Uingereza yaahidi msaada wa Pauni milioni 12 kwa ajili ya Pakistan.

https://p.dw.com/p/HpRs
Rais Asif Ali Zardari wa Pakistan.Picha: AP

Watu zaidi wameuawa leo kutokana na mapigano yanayoendelea katika bonde la Swat kaskazini-magharibi mwa Pakistan baina ya majeshi ya nchi hiyo na wapiganaji wa kitaliban.
Wakati huo huo rais Asif Ali Zardari amewasili mjini London kwa ajili ya kufanya mazungumnzo na waziri mkuu wa Uingereza Gordon Brown juu ya Pakistan.

Katika tukio jingine msemaji wa jeshi la Pakistan amefahamisha leo kwamba wanajeshi wanne wameuawa katika mapigano dhidi ya wapinzani wa kitaliban.

Katika mapambano hayo mataliban 10 pia waliuliwa.

Habari zaidi zinasema kuwa vikosi maalum vya jeshi la serikali ya Pakistan viliishambulia kambi ya mafunzo ya wapiganaji wa kitaliban kwenye bonde la Swat.

Wakati huo huo mkuu wa majeshi ya Pakistan ameyaagiza majeshi yake yajaribu kuepusha vifo vya raia hata kama kufanya hivyo kutawahatarisha wao wenyewe.Mkuu huyo Jenerali Ashfaq Kayani amewaambia askari wake waepushe vifo vya raia kwa kufanya mashambulio ya uhakika.

Na Uingereza imeahidi msaada wa Pauni milioni 12 kwa ajili ya Pakistan.Hapo awali rais Zardari alitoa mwito kwa jumuiya ya kimataifa iwasaidie watu zaidi ya milioni moja wa Pakistan wanaokabiliwa na maafa kutokana na mapambano ambayo leo yameingia katika siku ya 17.