1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rice ashinikiza ugavi wa madaraka nchini Kenya

18 Februari 2008
https://p.dw.com/p/D9KN

Waziri wa mashauri ya kigeni wa Marekni, Condoleezza Rice, amewataka viongozi wa kisiasa wanaozozana nchini Kenya wakubaliane kuhusu kugawana madaraka ili kuumaliza mgogoro wa kisiasa uliosababisha umwagaji damu nchini humo.

Condoleezza Rice amesema makubaliano ya ugavi wa madaraka yatauimarisha uhusiano kati ya Kenya na Marekani.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Nairobi leo baada ya kukutana na katibu mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan, Condoleezza Rice amesema Marekani haitaendelea na shughuli zake nchini Kenya kama kawaida mpaka mzozo wa kisiasa utanzuliwe.

Aidha Condoleeza Rice amesema Marekani itaendeleza uhusiano wa kirafiki na Kenya lakini akasisitiza hilo litafanyika iwapo Kenya itakuwa thabiti na yenye serikali halali inayoweza kuwaongoza wakenya wote.

Kabla waziri Rice kuwasili mjini Nairobi serikali ya rais Mwai Kibaki ilitoa taarifa ikisema haitakubali shinikizo la kuitaka ifikie makubaliano na kiongozi wa upinzani Raila Odinga.