1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ripoti kuhusu usalama wa Sudan yatolewa

Kabogo Grace Patricia27 Julai 2010

Ripoti hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon

https://p.dw.com/p/OVtC
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon.Picha: AP

Imeelezwa kuwa kuna hatari ya kuongezeka kwa hali ya kutokuwepo kwa amani nchini Sudan kutokana na kukosekana kwa mpango wa amani katika jimbo la Darfur na kuhusu kura ya maoni inayotarajiwa kufanyika Januari mwakani iwapo Sudan Kusini ijitenge na Sudan Kaskazini. Hii ni kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon.

Ripoti hiyo iliyotolewa mwanzoni mwa wiki hii imeeleza kuwa tathmini iliyofanywa kuhusu hali inayovikabili vikosi vya pamoja vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika-UNAMID vilivyoko katika jimbo lenye migogoro la Darfur, inaonyesha kuwa ghasia ziliibuka baada ya uchaguzi mkuu wa Sudan mwezi Aprili, mwaka huu. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon amesema ghasia ziliibuka kati ya vikosi vya usalama vya serikali na kundi la waasi la Justice and Equality Movement-JEM na kukiuka ahadi zao walizotoa za kusitisha mapigano katika makubaliano yaliyosainiwa mwezi Februari, mwaka huu na hivyo kuufanya mwezi wa Mei kuwa mwezi mbaya kabisa tangu kikosi cha UNAMID kilipoanzishwa mwaka 2007, kutokana na mauaji katika eneo hilo. Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lenye wanachama 15 jana lilitarajiwa kuijadili tathmini hiyo ya Bwana Ban. Wanadiplomasia wa baraza hilo wamesema kuwa mipango ya jopo ni kupitisha azimio baadaye juma hili la kukiongezea muda wa mwaka mmoja zaidi kikosi cha UNAMID, kama ambavyo Bwana Ban alishauri.

Katibu huyo mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema anahofu kuwa kitendo cha waasi wa JEM kujitoa katika mazungumzo ya Doha kunaweza kuleta athari katika taifa hilo na kuzitaka JEM na serikali ya Sudan kurejea haraka katika meza ya mazungumzo. Bwana Ban pia ameyashutumu makundi ya waasi katika jimbo la Darfur na serikali ya Sudan kwa kukizuia kikosi cha UNAMID katika maeneo ambako kumekuwa na mapigano. Ripoti hiyo imebainisha kuwa mwezi Mei peke yake UNAMID ilizuiwa katika matukio kumi, ambapo manane yalizuiliwa na serikali ya Sudan kwa sababu za kiusalama. Hata hivyo, balozi wa Sudan katika Umoja wa Mataifa ambaye anamaliza muda wake, Abdalmahmoud Abdalhaleem amesema kumekuwa hakuna vikwazo vyovyote hadi sasa vilivyowekwa na serikali ya Sudan dhidi ya kikosi cha UNAMID.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kati ya Julai mwaka uliopita na Julai mwaka huu, vikosi vya usalama vya kulinda amani vya UNAMID vilishambuliwa katika matukio 28 na kusababisha wanajeshi 10 kuuwawa na wengine 28 walijeruhiwa. Hali ya kibinaadamu pia bado ni mbaya huku watu milioni mbili ambao ni robo ya idadi ya watu wa Darfur wakiwa hawana makaazi na wanategemea msaada wa mashirika ya misaada kwa ajili ya kuishi. Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula-WFP, limekuwa likikabiliwa na ugumu wa kuwafikia watu wote wanaohitaji misaada katika jimbo la Darfur. Shirika hilo lilishindwa kuwafikia kiasi watu 250,000 mwezi Mei kutokana na ukosefu wa usalama. Bwana Ban amesema kuwa uhaba wa maji Darfur unazidi kuongezeka, huku idadi kadhaa ya visima vya maji vikikauka. Maafisa wa Umoja wa Mataifa wanakadiria kuwa kiasi watu 300,000 waliuawa Darfur tangu waasi walipoanzisha mapigano mwaka 2003, wakiituhumu serikali ya Sudan kwa kutolijali jimbo hilo. Hata hivyo serikali kwa upande wake imekuwa ikisisitiza kwamba idadi ya watu waliouawa ni 10,000.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (Reuters)

Mhariri:Josephat Charo