1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

-Rummenige aishambulia FIFA na Blatter ajizatiti kupambana na rushwa

29 Julai 2011
https://p.dw.com/p/Rd6T

Barani Afrika mashindano ya kombe la vilabu bingwa Jumamosi hii inaumana tena miamba ya Afrika kaskazini Esperance ya Tunisia, na Al-Ahly ya Misri katika mashindano ya ligi ya ubingwa wa Afrika. Esperance itakua ikicheza nyumbani mjini Tunis. Timu hizo mbili zilichuana katika nusu fainali mwaka jana ambapo bao la mkono lililofungwa na Mnigeria Michael Eneramo liliwapa ushindi Watunisia mbele ya mashetani hao wekundu wa Misri. Kwa hiyo bila shaka Al Ahly pamoja na kucheza ugenini itakuwa inawania kulinda heshima yake kabla ya mechi ya marudiano nyumbani Cairo.Katika mechi nyengine Wydad Casablanca ya Morocco wakiwa na mshambuliaji hatari, mzaliwa wa Congo, Fabrice Ondama, wataumana na Mouloudia ya Algeria mjini Casablanca.Timu nyengine katika mashindano hayo ni Enyimba ya Nigeria, Al Hilal ya Sudan, Coton sport Garoua ya Cameroun.

Fussball FC Bayern München Karl-Heinz Rummenigge
Mkuu wa kilabu ya Bayern Munich Karl-Heinz RummeniggePicha: picture-alliance/dpa

Katika kandanda la Ulaya, mchezaji wa zamani wa kimataifa wa Ujerumani, Karl Heinz Rummenigge, amewashambulia vikali viongozi wa soka akitaka vilabu viwe na usemi mkubwa katika uendeshaji wa mchezo huo. Rummenigge ambaye ni mwenyekiti wa chama cha vilabu vya Ulaya na mkuu wa kilabu kubwa katika ligi ya Ujerumani-Bundesliga ya Bayern Munich- aliliambia gazeti la "The Guardian" la Uingereza kwamba amepoteaza imani na shirikisho la kandanda barani ulaya ,FIFA, kutokana na mlolongo wa kashfa za hivi karibuni.

Kwa upande mwengine akizungumza wiki hii mjini Rio de Janeiro Brazil, kiongozi wa FIFA Sepp Blatter amesema tena kwamba hawatakuwa wavumilivu katika vita dhidi ya rushwa ambayo imeuandama mchezo wa kandanda. Blatter alitoa matamshi hayo siku tatu baada ya mshirika wa zamani aliyekua mkuu wa shirikisho la soka barani Asia Mohamed bin Hammam kufungiwa kushiriki katika shughuli za kanadanada maisha kwa sababu ya rushwa. Pia Rais huyo wa FIFA alikanusha madai ya Hammam kwamba Blatter ni dikteta akisema hachukuwi maamuzi peke yake. Pia alisema vita vyake havitakuwa dhidi ya rushwa pekee bali , utumiaji madawa yaliopigwa marufuku ya kuimarisha nguvu mwilini pamoja na uabaguzi katika kandanda.

FIFA Wahlen Präsident Joseph Blatter
Rais wa FIFA Joseph (Sepp) BlatterPicha: dapd

Nchini Uingereza katika ligi kuu ya England Premier League, kocha mpya wa Chelsea , mreno Villa Boas anasema anajua kwamba timu yake ina wachezaji wakongwe mno lakini ana mipango ya kuwekeza zaidi kwa vijana.Kocha huyo aliyechukua nafasi ilioachwa na Carlo Ancelotti kutoka Italia mwezi uliopita aliuambia mkutano na waandishi habari kwamba sio tu Chelsea ina wachezaji wakongwe lakini ni miongoni mwa zile kongwe katika ligi kuu ya England .Tayari kilabu hiyo imemsajili Thibault Courtois kabla ya kuwapa kipa huyo wa Ubeligiji , kilabu Athletico Madrid kwa mkopo. Pia imefikia makubaliano na mchezaji chipukizi wa kiungo Oriol Romeu kutoka Barcelona.

Mwandishi: Mohamed Abdul-Rahman/afp,rtr

Mhariri:Miraji Othman