1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Shambulio la Israel Damascus lauwa makamanda wa Iran

Iddi Ssessanga
20 Januari 2024

Iran imethibitisha vifo vya askari maafisa wake kadhaa wa kikosi maalumu cha ulinzi wa mapinduzi, IRGC, katika mashambulizi dhidi ya mji wa Damascus, Syria, wakiwemo washauri wawili wa ngazi ya juu, na kuilaumu Israel.

https://p.dw.com/p/4bUhx
Syria | Wafanyakazi wa uokoaji baada ya shambulio la anga la Israel mjini Damascus
Shughuli ya uokozi ikiendelea baada ya shambulio la anga la Israel mjini Damascus, Januari 20, 2024.Picha: LOUAI BESHARA/AFP/Getty Images

Shambulio la Israel mjini Damascus limemuua mkuu wa kijasusi wa kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Iran nchini Syria na naibu wake pamoja na walinzi wengine wawili siku ya Jumamosi, vyombo vya habari vya Iran viliripoti.

"Mkuu wa Idara ya Upelelezi ya Walinzi wa Mapinduzi ya Syria, naibu wake na walinzi wengine wawili wameuawa mashahidi katika shambulio la Israel dhidi ya Syria," shirika la habari la Iran la Mehr lilisema, likinukuu chanzo cha habari lakini ambacho hakikutajwa.

Katika taarifa yake, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi limethibitisha kuwa wanachama wake wanne wameuawa katika shambulio la mji mkuu wa Syria na kuishutumu Israel kwa kuhusika na shambulio hilo.

Shirika rasmi la habari la Syria SANA limesema jengo la makazi katika kitongoji cha Mazzeh mjini Damascus lililengwa kwa kile lilichokiita "uchokozi wa Israel".

Soma pia: Israel yafanya shambulio katika bandari ya Syria

Shirika la uchunguzi wa vita la Syrian Observatory for Human Rights limesema shambulio hilo la Israel limelenga  maeneo ya jirani yanayowahifadhi viongozi wa kikosi cha walinzi wa mapinduzi, pamoja na makundi yanayowaunga mkono Wapalestina.

Katika wiki za hivi karibuni, Israel imeshutumiwa kwa kuzidisha mashambulizi dhidi ya viongozi waandamizi wa Iran na washirika wake nchini Syria na Lebanon - waungaji mkono wa kundi la wanamgambo wa Kipalestina la Hamas -- jambo linalozusha hofu kwamba mzozo wa Gaza unaweza kupanuka.

Syria | Wafanyakazi wa uokoaji baada ya shambulio la anga la Israel mjini Damascus
Israel imekuwa ikifanya mashambulizi yanayolenga wanajeshi na makundi yanayoiunga mkono Iran nchini Syria, tangu kuanza kwa vita yva wenyewe kwa wenyewe nchini humo.Picha: LOUAI BESHARA/AFP/Getty Images

Uvamizi huo wa Israel unakuja siku nne baada ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi kusema kuwa lilishambulia "makao makuu ya kijasusi ya Israel" mjini Arbil, mji mkuu wa jimbo la Kurdistan kaskazini mwa Iraq. Maafisa wa Iraq walisema shambulizi hilo liliua raia wanne na kuwajeruhi wengine sita.

Israel yakataa kuzungumzia shambulizi hilo

Lilipoulizwa kuhusu shambulizi hilo, jeshi la Israel liliiambia AFP: "Hatutoi maoni yoyote kuhusu ripoti kutoka kwa vyombo vya habari vya kigeni".

Wakati wa zaidi ya muongo mmoja wa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria, Israel imefanya mamia ya mashambulizi ya angani katika ardhi yake, hasa yakilenga vikosi vinavyoungwa mkono na Iran na pia maeneo ya jeshi la Syria.

Lakini imezidisha mashambulizi tangu vita kati ya Israel na Hamas, ambayo kama vile vuguvugu la Lebanon la Hezbollah ni mshirika wa Iran, kuanza Oktoba 7.

Shirika la Observatory lilisema "shambulio la kombora la Israeli lililenga jengo la ghorofa nne, na kuua watu sita ... na kuharibu jengo zima ambako viongozi wa Iran walikuwa wakikutana" huko Damascus. Mkurugenzi wake, Rami Abdel Rahman, alisema mmoja wa waathirika alikuwa raia wa Syria.

Shirika hilo la ufuatiliaji wa vita vya Syria lenye makao yake makuu nchini Uingereza na mtandao wa vyanzo vya habari ndani ya Syria walisema jengo lililolengwa ni la IRGC na kwamba kitongoji hicho kinajulikana kuwa eneo lenye ulinzi mkali wa viongozi wa IRGC na makundi ya Wapalestina wanaoiunga mkono Iran.

Soma pia: Syria yatishia kujibu mashambulizi ya Israel

Eneo la Mazzeh pia ni nyumbani kwa makao makuu ya Umoja wa Mataifa, balozi na mikahawa. "Kwa hakika yalikuwa yanawalenga wanachama wakuu" wa vikundi vinavyoungwa mkono na Tehran au vikosi vya Iran, Abdel Rahman aliiambia AFP.

Syria | Wafanyakazi wa uokoaji baada ya shambulio la anga la Israel mjini Damascus
Vikosi vya uokoaji na usalama vikikusanyika katika eneo la shambulio lililoripotiwa kufanywa na Israeli mjini Damascus Januari 20, 2024.Picha: LOUAI BESHARA/AFP/Getty Images

Maasfisa wa Iran waliouawa na Israel

Mnamo mwezi Disemba, shambulio la anga la Israel lilimuua jenerali mkuu wa Iran nchini Syria, jeshi lilisema.

Razi Moussavi alikuwa kamanda mkuu wa operesheni za nje za kikosi cha ulinzi wa mapinduzi cha Quds, aliyeuawa nje ya Iran tangu shambulio la droni za Marekani mjini Baghdad Januari 3, 2020 kumuua kamanda wa Kikosi hicho, Qasem Soleimani.

Katika mwezi huo huo, mashambulizi ya anga mashariki mwa Syria, ambayo yanadhaniwa kufanywa na Israel, yaliwauwa takriban wapiganaji 23 wanaoiunga mkono Iran, shirika la Observatory lilisema wakati huo, likiripoti kuuawa kwa wengine wanne kaskazini mwa nchi hiyo.

Miezi ya hivi karibuni pia imeshuhudia mapigano ya mara kwa mara ya kuvuka mpaka kati ya Israel na Hezbollah kusini mwa Lebanon.

Israel haitoi maoni yoyote juu ya mashambulizi mmoja mmoja yanayolenga Syria, lakini mara kwa mara imesema haitaruhusu adui mkuu Iran, ambayo inaiunga mkono serikali ya Rais Bashar al-Assad, kupanua uwepo wake huko.

Tangu mwaka 2011, Syria imekuwa ikikabiliwa na mzozo wa umwagaji damu ambao umegharimu maisha ya zaidi ya nusu milioni na kusababisha mamilioni ya watu kuyahama makazi yao.