1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Shambulio la Urusi lauwa watu 51 Kharkiv, Ukraine

6 Oktoba 2023

Shambulio la Alhamisi la Urusi limeua takriban watu 51 waliokuwa wamekusanyika msibani katika kijiji cha Groza katika mji wa Kharkiv mashariki mwa Ukraine, na kuibua hasira kutoka kwa viongozi wa nchi za Magharibi.

https://p.dw.com/p/4XB55
Ukraine Krieg Raketenangriff auf das Dorf Hroza, Region Kupyansk
Picha: Ukrainian Presidential Press Office/AP Photo/picture alliance

Waandishi wa shirika la habari la AFP waliokuwa eneo la tukio walishuhudia miili kadhaa iliyoungua ikiwa imevalia nguo za kiraia huku waokoaji wakibeba maiti kutoka kwenye vifusi huku maiti nyingine zikihifadhiwa kwenye mifuko mieupe.

Vikosi vya uokoaji vimethibitisha idadi ya vifo na kusema miongoni mwa waliouawa ni mtoto aliyezaliwa mwaka 2017. Watu wengine 6 wamejeruhiwa.   

Watu hao waliouawa walikuwa wakiomboleza kifo cha mpendwa wao katika mgahawa. Watu wengine kadhaa wamepoteza maisha katika duka moja lililopo katika jengo moja katika kijiji cha Groza, chenye idadi ya watu 330, kaskazini mashariki mwa  mkoa wa Kharkiv.

Kulingana na msemaji wa ofisi ya mwendesha mashtaka wa eneo hilo Dmytro Tchoubenko, aliyenukuliwa na shirika la habari la Interfax-Ukraine, msiba huo ulikuwa wa mwanajeshi wa Ukraine aliyekufa katika mapigano, ambaye pia mwanawe-mwanajeshi, na mkewe waliangamia katika shambulio hilo.   

Russischer Militärangriff in der Region Charkiw
Kikosi cha zimamoto wakiwa eneo kulikotokea shambulio hilo, Kharkiv Ukraine: 05.10.2023Picha: OLEH SYNIEHUBOV/REUTERS

Volodymyr Mukhovaty, mwenye umri wa miaka 70, ameliambia shirika la habari la AFP: "Mwanangu alipatikana bila kichwa, bila mikono, bila miguu, bila chochote. Walimtambua kutokana na nyaraka zake."     

Soma pia: Viongozi 50 wa Ulaya kusisitiza uungaji mkono kwa Ukraine

Mukhovaty ameendelea kusema kuwa mke na binti yake walikuwa pia wakihudhuria mkesha huo wa maombolezo na ingawa alikuwa na matumaini kidogo ya kuwapata wakiwa hai, aliwatazama waokoaji kwa mbali huku akijawa na hofu na kusema: "Niliishi na mke wangu kwa miaka 48, sitadumu kwa muda mrefu peke yangu."

Viongozi mbalimbali walaani shambulio hilo

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky, ambaye kwa sasa yupo nchini Uhispania kuhudhuria mkutano wa viongozi wa Ulaya, amelaani "shambulio la kigaidi lisilo la kibinadamu" dhidi ya mji huo ulioko katika mkoa wa Kharkiv, karibu na Kupiansk, na ambao mara kwa mara hulengwa na mashambulizi ya Urusi. 

Granada Treffen Scholz und Selenskyj
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky (Kulia) akisalimiana na Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz mjini Grenada, Uhispania :05.10.2023Picha: UKRAINIAN PRESIDENTIAL PRESS/AFP

Wakati wa mkutano na  Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz,  Zelensky amesema inawezekana tu kuwalinda watu dhidi ya mashambulizi kama hayo kwa kupewa msaada wa ulinzi wa anga huku akizungumzia pia msaada kutoka Marekani wa mfumo mpya wa ulinzi wa Patriot.

Mkuu wa diplomasia ya Umoja wa Ulaya Josep Borrell ameandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X ( iliyokuwa zamani Twitter): "Shambulio la umwagaji damu dhidi ya Groza, linadhihirisha kuwa ukatili wa Urusi umefikia kiwango cha juu zaidi".       

Msemaji wa Ikulu ya  White House  Karine Jean-Pierre, amekitaja kitendo hicho kuwa "kibaya" na kusema: "Ni lazima tuendelee kuwaunga mkono watu wa Ukraine kwa sababu ya hali mbaya wanaishi kila siku". Kauli hiyo inajiri wakati Rais Joe Biden anajaribu kupata fedha za ziada kutoka kwa Baraza la Congress ili kuisaidia Ukraine.

USA UN-Generalversammlung in New York Annalena Baerbock
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Annalena BaerbockPicha: Thomas Trutschel/photothek/picture alliance

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Annalena Baerbock amesema siku ya Alhamisi kuwa Ujerumani itafanya kila liwezekanalo ili Ukraine iwe na uwezo wa kujikinga na ugaidi wa makombora ya Putin.

Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak amesema kwa upande wake kuwa shambulio hilo linaonesha wazi kiwango cha ukatili kinachoweza kufikiwa na vikosi vya Urusi.

Kulingana na taarifa za awali, shambulio hilo lilitekelezwa kwa kutumia kombora la masafa marefu "Iskander" lililoharibu kabisa duka na mgahawa uliokuwa katika jengo moja wakati takriban watu 60 walikuwa msibani, ameeleza Waziri wa Ulinzi Igor Klymenko kwenye televisheni ya taifa.

(AFP)