1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Shirika la kutetea Haki za Binadamu la Human Rights watch laipongeza mahakama ya Umoja wa Mataifa ya Sierra Lione.

Scholastica Mazula29 Mei 2008

Mahakama ya Kimataifa ya makosa ya kivita ya Nchini Sierra Lione imewaongezea muda wa vifungo Washitakiwa wa makosa ya uhalifu wa kivita vilivyomalizika nchini humo mwaka 2002.

https://p.dw.com/p/E8qp
Mkurugenzi mtendaji wa Human Rights Watch, Kenneth Roth.Picha: AP

Uamuzi uliochukuliwa na Mahakama maalumu ya makosa ya kivita ya Sierra Leone wa kukataa kuwapunguzia hukumu wanamgambo wawili waliotiwa hatiani kwa kosa la kushiriki mapigano waliyoyaita ya haki, ni uamzi sahihi katika kuthihirisha haki kwa waathirika wa mapigano hayo.

Hii ni kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na Shirika la Kimataifa la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch.

Mahakama ya rufaa ya Umoja wa Mataifa ya Sierra Leon , ilitoa maamuzi hayo Mei, ishirini na nane, dhidi ya watuhumiwa, Moinina Fofana na Allieu Kodewa.

Watuhumiwa hao wawili walikuwa ni viongozi wa majeshi ya raia waliokuwa wakiungwa mkono na Serikali ya rais wa zamani wa nchi hiyo Ahmad Tejan Kabbah, wakati wa mapigano ya kinyama yaliyotokea nchini humo mwaka 1991 na kumalizika mwaka 2002.

Watu hao wawili wanatuhumiwa kuwa walihusika katika matukio ya kivita na kushiriki moja kwa moja vitendo kama vile mauaji ya raia.

Mahakama ya ndani nchini Sierra Leon, iliwapunguzia hukumu watu hao kutokana na kujihusisha kwao katika mgogoro wa kulinda Demokrasia wakati huo huo Mahakama ya Rufaa ya Umoja wa Mataifa imekataa sehemu ya maamuzi hayo.

Kwa kuzingatia makosa yao ya kwanza na haya ambayo yamepatikana , mahakama ya rufaa imeongeza hukumu ya Fofana kutoka miaka sita hadi kumi na tano na Kodewa kutoka miaka nane hadi miaka ishirini.

Mshauri wa masuala ya haki wa Shirika la Human Rights Watch, Elise Kepple, anasema kwamba uamuzi huo unaonyesha wazi kwamba hakuna msamaha wowote utakaotolewa kwa mtu anayefanya vurugu za kuwashambulia raia na kuwatendea vitendo vya kinyama bila kuangalia ni sababu gani zilizochangia mtu huyo kufanya vitendo hivyo.

Anasema mahakama hiyo maalumu imekuwa ni muhimu sana kwa ajili ya kurejesha haki kutokana na matendo ya kinyama yaliyofanyika nchini Sierra Lione.

Kopple, anasisitiza kuwa uamuzi huu unaleta changamoto na kuongeza hatua mbele na kuambukiza maamuzi kama hayo kwa mahakama nyingine za makosa ya jinai za Kimataifa.

Mahakama hiyo maalumu, imewashitaki na kuwapeleka kwenye vyombo vya haki wale wote waliohusika kwa kiasi kikubwa katika matukio hatari tangu mwezi Novemaba mwaka 1996.

Matukio hayo ni pamoja na ya kivita, ukiukwaji wa haki za binadamu na matukio mengine hatari.

Mahakama Maalumu ya Sierra Lione, iliundwa mwaka 2002 kupitia makubaliano baina ya Serikali ya nchi hiyo na Umoja wa Mataifa na malengo ya mahakama hiyo ni kuleta muundo mpya wa upatikanaji wa haki Kimataifa.

Mahakama hiyo imegundua kuwa watuhumiwa hao walijihusisha katika vurugu mbaya sana na uvunjaji wa haki za binadamu, kufuatia ushahidi uliotolewa na zaidi ya watu mia moja.

Zaidi ya watu elfu hamsini waliuawa katika vita hivyo vya wenyewe kwa wenyewe.