1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Solana autembelea Ukanda wa Gaza

Charo Josephat/ DPAE27 Februari 2009

Umoja wa Ulaya kusaidia kuujenga upya ukanda wa Gaza

https://p.dw.com/p/H2i1
Kiongozi wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Javier SolanaPicha: AP

Kiongozi wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Javier Solana, amezuru Ukanda wa Gaza hii leo. Wakati huo huo, umoja huo umeahidi kutoa kitita cha dola milioni 556 kwenye mkutano wa kimataifa wa kuifadhili Palestina utakaofanyika Jumatatu ijayo nchini Misri.

Javier Solana amesema ameutembelea Ukanda wa Gaza hii leo kuonyesha mashikamano na wakaazi wa ukanda huo. Solana ameyasema hayo wakati alipozungumza na waandishi wa habari katika shule ya Marekani huko Beit Lahiya iliyoharibiwa wakati wa harakati za jeshi la Israel iliyodumu siku 22.

"Nimekuja hapa leo kuonyesha mshikamano na wananchi wa Ukanda wa Gaza na kuwaambia kwamba tutawasaidia katika kazi ya kuujenga upya ukanda huu."

Solana pia amesema Umoja wa Ulaya unayaunga mkono mazungumzo ya kutafuta umoja kati ya makundi hasimu ya kisiasa ya Kipalestina yanayozozana, lakini amesisitiza kwamba msimamo wa mwisho wa Umoja wa Ulaya utategemea makubaliano yatakayofikiwa kati ya pande hizo.

Shirika la habari la Kipalestina la Wafa limesema waziri wamashauri ya kigeni wa Norway, Jonas Gahr Stoere, pia ameutembelea Ukanda wa Gaza leo Ijumaa. Shirika la habari limeripoti kwamba maafisa hao wawili wa Ulaya wameelezea kushutushwa na ukubwa wa uharibifu uliosabishwa na mashambulio ya angani, ardhini na baharini yaliyofanywa na jeshi la Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza.

Waziri Jonas Gahr wa Norway amesema, "Huu ni uharibifu usio na maana. Kuyaharibu maisha ya wananchi wa kawaida, kusababisha mateso na kutojenga amani na kutodumisha usalama." Aidha kiongozi huyo amesema wanamgambo wa kipalestina wanaovurumisha maroketi nchini Israel wanabeba dhamana kubwa kwa kusababisha vita hivyo, lakini aina ya uharibifu uliofanywa na Israel unavuka mipaka ya sheria za kimataifa.

Wakati huo huo, Javier Solana amesema Umoja wa Ulaya uko tayari kupeleka waangalizi wake katika kivuko cha Rafah kati ya Ukanda wa Gaza na Misri kama ilivyotakiwa kwenye mkataba wa mwaka 2005 kati ya Israel na mamlaka ya ndani ya Wapalestina. Hata hivyo, hatua hiyo itachukuliwa mara tu Wapalestina watakapokubaliana wenyewe kwa wenyewe ni nani atakayekisimamia kivuko hicho cha Rafah.

Ziara ya Javier Solana katika Ukanda wa Gaza imefanyika siku chache kabla mkutano wa kimataifa wa ufadhili kwa ajili ya Gaza uliopangwa kufanyika Machi 2 katika mji wa mapumziko wa Sharm el Sheikh nchini Misri. Mamlaka ya ndani ya Palestina inahitaji dola bilioni 2.8 kujenga upya kile kilichoharibiwa na Israel katika Ukanda wa Gaza.

Solana amesema Umoja wa Ulaya utatoa kiwango cha dola milioni 556, ikiwa ni sawa na yuro milioni 436, kwa ajili ya kuujenga upya ukanda huo. Tangazo rasmi, hata hivyo, litatolewa kwenye mkutano wa Sharm el Sheikh Jumatatu ijayo.

Kiongozi huyo wa Umoja wa Ulaya baadaye anatarajiwa kusafiri kwenda mjini Ramalllah, Ukingo wa Magharibi wa mto Joran, kukutana na rais wa mamlaka ya ndani ya Wapalestina, Mahmoud Abbas, na mjumbe maalum wa Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati, George Mitchel. George Mitchel anatarajiwa kukutana na rais Abbas leo usiku mjini Ramallah.

Javier Solana amewasili Gaza baada ya kuzitembelea Syria, Lebanon, Misri na Israel, katika ziara yake ya kidiplomasia ya wiki nzima huko Mashariki ya Kati.