1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

TEHRAN:Iran yaendelea kuwahoji wanamaji wa Uingereza

27 Machi 2007
https://p.dw.com/p/CCF6

Iran imeendelea kuwahoji askari 15 wa majini wa Uingereza iliyowakamata wiki iliyopita baada ya kuingia katika eneo la nchi hiyo.

Balozi wa Uingereza nchini Iran amekuwa na mazungumzo katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, ambapo mjini London Balozi wa Iran nchini Uingereza naye ameitwa katika Wizara ya Nje juu ya suala hilo.

Serikali ya Iran imemthibitishia Balozi wa Uingereza nchini humo Geofrey Adams kuwa wanamaji hao wako salama .

Uingereza imekuwa ikadai kufahamishwa walipo askari hao na kutaka waachiwe mara moja kwani walikuwa katika doria za kiulinzi.Lakini Iran imesisitiza kuwa waliingia katika eneo la nchi hiyo bila ya ruhusa.

Wakati huo huo katika kile kinachoonekana kuiunga mkono Uingereza Iraq imesema kuwa askari hao walikamatwa katika eneo la Iraq na siyo Iran.

Waziri wa mambo ya Nje wa Iraq Hoshyar Zebar aliwasiliana kwa simu na mwenziye wa Iran Manouchehr Motakki akimuelezea kuwa wanamaji hao walikuwa katika eneo la Iraq na kutaka waachiwe.