1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

TEL AVIV: Wanamgambo wa Hamas wavurumisha makombora mjini Sderot

28 Mei 2007
https://p.dw.com/p/CBxL

Wanamgambo wa kipalestina wamevurumisha makombora kusini mwa Israel mapema leo. Kombora moja limeanguka katika mji wa Sderot, ambao ni nyumbani kwa waziri wa ulinzi wa Israel, Amir Peretz.

Shambulio hilo limefanywa wakati waziri huyo alipokuwa mjini humo akipiga kura katika uchaguzi wa mashinani wa chama cha Labour.

Msemaji wa jeshi la Israel amethibitisha kuwa makombora matatu yameanguka mjini Sderot leo asubuhi ikiwa ni siku moja tangu roketi aina ya Qassam kumuua muisraeli aliyekuwa na umri wa miaka 35 mjini humo.

Mji wa Sderot unapatikana kilomita 5 kaskazini mashariki mwa Ukanda wa Gaza na umekabiliwa na mashambulio ya maroketi zaidi ya 250 yaliyovurumishwa kutoka eneo la pwani katika wiki mbili zilizopita.

Wakati haya yakiarifiwa, wanamgambo wa Hamas wameapa hawatakomesha mashambulio ya maroketi dhidi ya Israel licha ya onyo kali lililotolewa na waziri mkuu wa Israel, Ehud Olmert akisema kwamba operesheni ya kuwachakaza wanagambo hao itaendelea.

Ehud Olmert pia alisema mtu yeyote atakayejihusisha na ugaidi hana ulinzi wowote. Vitisho hivyo vinafuatia usiku wa mashambulio ya angani yaliyofanywa na jeshi la Israel dhidi ya ngome za Hamas katika Ukanda wa Gaza. Hakuna ripoti za majeruhi zilizotolewa.