1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

TIKRIT, IRAQ: Mamia ya waombolezaji wazuru kaburi la rais wa zamani wa Iraq, Saddam Hussein.

1 Januari 2007
https://p.dw.com/p/CCeB

Mamia ya waombolezaji wamelizuru kaburi la Rais wa zamani wa Iraq, Saddam Hussein ambapo walimwombea dua na kuahidi kulipiza kisasi cha kunyongwa kwake.

Saddam Hussein alizikwa jana alfajiri katika kijiji cha Awja, karibu na Tikrit, kaskazini mwa Iraq, saa kadhaa baada ya kutiwa kitanzi.

Katika mji wa Jenin, kwenye Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan wapalestina zaidi ya alfu moja waliandamana mabarabarani kumwomboleza Saddam Hussein.

Mahakama ya Iraq mwezi uliopita ilimuhukumu mtawala huyo wa zamani wa kiimla aliyekuwa na umri wa miaka sitini na tisa, adhabu ya kifo kwa mauaji ya mwaka 1982 ya watu takriban 150 katika mji wa Dujail ambao wakazi wake wengu ni wa madhehebu ya Shia.

Wakati huo huo; wizara ya ulinzi ya Marekani imetangaza kwamba idadi ya wanajeshi wa Marekani waliouawa nchini Iraq tangu vita vilipoanza mwaka 2003 imefikia wanajeshi 3,000.

Kwa mujibu wa wizara hiyo ya ulinzi mwezi uliopita ndiyo mwezi ambao umekuwa hatari zaidi kwa wanajeshi wa Marekani tangu walipoingia nchini Iraq.