1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

091011 Merkel Sarkozy

10 Oktoba 2011

Kuanguka kwa Ugiriki kiuchumi kunakwenda sambamba na benki ambazo zimeshikilia dhamana za nchi barani Ulaya, jambo ambalo hapo jana jioni (09.10.2011) liliwakutanisha Kansela Angela Merkel na Rais Nikolas Sarkozy.

https://p.dw.com/p/12ooJ
Kansela Angela Merkel (kushoto) na mgeni wake Rais Nicolas Sarkozy mjini Berlin.
Kansela Angela Merkel (kushoto) na mgeni wake Rais Nicolas Sarkozy mjini Berlin.Picha: dapd

Inapobidi viongozi wa mataifa mawili makubwa yanayoongoza kiuchumi kwenye Umoja wa Ulaya kukutana, ni wazi kuwa mambo yamefika pabaya. Na wote wawili, Kansela Merkel na Rais Sarkozy, hawakulificha hilo jioni ya jana, kwa kusisitiza dhima ya uongozi wa kisiasa kutatutua mkwamo uliopo.

"Tumedhamiria kufanya kila linalowezekana kuzisaidia kifedha benki zetu, maana suala la mgogoro wa madeni ni la msingi sana kwa maendeleo mazuri ya kiuchumi." Kansela Merkel aliwaambia waandishi wa habari jioni ya jana baada ya mazungumzo na Rais Sarkozy.

Lakini inakuwaje benki zinazoporomoka zipatiwe fedha nyengine zaidi? Majibu ya swali hili yanabakia kwa Kansela Merkel na Rais Sarkozy, hali kila mmoja akiwa na mtazamo wake.

Undani wake utafanyiwa kazi mapema iwezekavyo kabla ya mkutano wa mataifa 20 yenye nguvu kiuchumi huko kwenye mji wa Cannes, Ufaransa, mwanzoni mwa mwezi ujao. Ukiacha hilo, viongozi hao wa Ufaransa wa Ujerumani, wanakubaliana juu ya wajibu wao kwa bara la Ulaya.

Kwa mfano kwenye suala la Ugiriki, Kansela Merkel na Rais Sarkozy, wamethibitisha tena mshikamano wao na nchi hiyo inayozidi kuporomoka kiuchumi.

"Tupo kwenye mawasiliano ya mara kwa mara na Troika. Ugiriki ni sehemu ya kanda ya euro na tutapata suluhisho, ambalo litaleta utulivu wa kifedha barani Ulaya kwa kiwango kile kile ambacho litatatua matatizo ya Ugiriki." Amesema Rais Sarkozy.

Kansela Angela Merkel (kulia) na Mkurugenzi Mkuu wa IMF, Christine Lagarde.
Kansela Angela Merkel (kulia) na Mkurugenzi Mkuu wa IMF, Christine Lagarde.Picha: dapd

Maneno haya yamekuja kurudisha moyo kidogo katika masoko ya hisa, baada ya wakaguzi wa mahisabu kutoka pande tatu, yaani Troika: Benki Kuu ya Ulaya, Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Kamisheni ya Umoja wa Ulaya, kuibua tena wasiwasi wao juu ya mwenendo wa mageuzi ya kiuchumi ya Ugiriki.

Kiongozi wa ujumbe wa IMF kwa Ugiriki, Paul Mathias Thomson, alisema hapo mwishoni mwa wiki kwamba Ugiriki inapiga hatua mbili mbele, huku ikirudi nyengine nyuma.

Wakati bado wakaguzi hawa wa pande tatu hawathibitisha ikiwa ama Ugiriki ipokee sehemu ya mkopo uliobakia wa euro bilioni nane au la, tayari maswali yanaulizwa ni kwa namna deni hili la Ugiriki litafidiwa. Hadi sasa inatajwa asilimia 60.

Jambo hilo, hata hivyo, linayaweka hatarini masoko ya hisa na kuzua shaka juu ya benki gani zitakazoweza kuchukuwa dhamana ya mabilioni ya mkopo wa Ugiriki. Kuhusiana na hali ya wasiwasi, Kansela Merkel na Rais Sarkozy wamepanga kukutana tena kabla ya mkutano wa Cannes, ili kuja na dira mpya ya Ulaya.

"Ujerumani na Ufaransa zitakuja na pendekezo, ambalo litatoa muongozo wa kufanya kazi pamoja katika masuala ya fedha na uchumi ya mataifa ya Ulaya. Jambo hili pia litajumuisha ubadilishaji wa mkataba." Amesema Kansela Merkel.

Linalohusika hapa si kuinusuru sarafu ya euro tu, bali pia kuonesha muelekeo wa Umoja wa Ulaya. Na hilo ndilo linalowaleta pamoja Kansela Merkel na Rais Sarkozy: kwamba tatizo hili halipaswi kuendelea zaidi ya hapa lilipokwishafika.

Kama alivyosema pia Rais wa Benki ya Dunia, Robert Zoellick, hapo mwishoni mwa wiki, alipomtaka Kansela Merkel kuchukuwa uongozi wa suala hili, "wakati wa kukwepakwepa umepita".

Mwandishi: Sabine Kinkartz/ZPR
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Thelma Mwadzaya