1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ubalozi wa Norway nchini Afghanistan wafungwa

11 Februari 2008
https://p.dw.com/p/D5eV

Ubalozi wa Norway nchini Afghanistan umefungwa kwa siku ya pili mfululizo hii leo kufuatia kitisho cha kushambuliwa.

Kitisho hicho kimetolewa kabla mwezi mmoja kumalizika tangu waziri wa mashauri ya kigeni wa Norway alipoponea chupuchupu katika shambulio dhidi yake mjini Kabul.

Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya Norway amesema ni mapema kusema ni lini ubalozi huo utakapofunguliwa.

Hata hivyo msemaji huyo amekataa kutoa maelezo ya kina kuhusu kitisho kilichosababisha ubalozi wa Norway mjini Kabul kufungwa hapo jana.

Haijabainika ikiwa wafanyakazi wamehamishwa kutoka jengo la ubalozi na hatua za usalama zilizochukuliwa.

Ubalozi wa Norway mjini Kabul umefungwa majuma kadhaa baada ya mwandishi wa habari wa Norway kuuwawa katika shambulio la kundi la Taliban lililofanywa na mshambuliaji wa kujitoa muhanga maisha dhidi ya hoteli moja ya kifahari mjini Kabul.

Watu wengine saba waliuwawa katika hujuma hiyo iliyofanywa wakati waziri wa mambo ya kigeni wa Norway alipokuwa katika hoteli hiyo.