1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi wa mapema wa bunge ndio suluhisho kwa mzozo wa siasa nchini Uturuki.

2 Mei 2007

Mahakama ya Kikatiba katika Uturuki imeibatilisha duru ya kwanza ya uchaguzi wa urais iliofanyika bungeni ijumaa iliopita. Kuweko wabunge 367 katika kikao hicho ndio sababu kuu iliotolewa na mahakama, kwani idadi hiyo haitoshelezi. Kuweza kuchagua rais ni lazima thuluthi mbili ya wabunge wote 550 waweko katika duru mbili za mwanzo. Hivyo, sasa hata duru ya pili ya uchaguzi, iliotazamiwa kufanywa leo, imefutiliwa mbali, na kuna mpango ya kuitisha uchaguzi wa mapema wa bunge.

https://p.dw.com/p/CB4L
Waziri mkuu wa Uturuki, Tayyip Erdogan(kulia), akisheherekea baada ya kutangazwa Abdullah Gül( kushoto) kuwa mtetezi wa urais wa nchi hiyo.
Waziri mkuu wa Uturuki, Tayyip Erdogan(kulia), akisheherekea baada ya kutangazwa Abdullah Gül( kushoto) kuwa mtetezi wa urais wa nchi hiyo.Picha: AP

Pindi idadi hiyo ya wabunge inakosekana, basi zoezi la uchaguzi wa urais haliwezi kuanza. Hivyo ndivyo ilivoamua mahakama kuu. Ni wazi kwamba mabishano haya kama Uturuki ibakie kuwa na serekali isioelemea dini au la yamegeuka kuwa ni mzozo wa nchi. Haisaidii kitu sasa kutafuta nani mwenye makosa wa haya yaliotokea. Jee makosa yako kwa Wa-Conservative wenye itikadi za kidiini waliomzunguka waziri mkuu Tayyip Erdogan na walio na wingi karibu ya thuluthi mbili bungeni- watu wanaoitawala nchi kama ya chama kimoja tu, tena waliokuwa hawajachukuwa juhudi yeyote ya kuregenza kamba? Lakini pia hata mtetezi wa urais aiyeshindwa, waziri wa sasa wa mambo ya kigeni, Abdullah Gül, licha ya kufanya kazi nzuri ya kuendeleza uhusiano wa nchi yake na nchi nyingine, bado hajaweza kukubalika kwa urahisi na watu wasioelemea dini. Sababu walioitoa watu hao ni itikadi zake za kidini za hapo kabla na kwamba mke wake anavaa mtandio.

Lakini jee Chama cha upinzani cha Social Democratic na vingine havibebi dhamana ya hali hii ya sasa? Vyama hivyo kwa miaka vimebakia vimesambaratika na kuzubaa kuwasilisha kwa wananchi programu na pia mwanasiasa mbadala aliye na heba na uchangamfu. Au: jee makosa yako kwa jeshi ambalo lilitoa tangazo kali la kuonya kwamba taasisi hiyo ndio ilio na jukumu la kuwa mlinzi wa mfumo wa dola isioelemea dini katika Uturuki?

Uamuzi wa mahakama, angalau kwa sasa, umetuliza mambo. Maandamano ya karibuni ya mamia kwa maelfu ya wananchi waliopinga kuchaguliwa kwa Abdullah Gül kama rais, na wakati huo huo kupinga wazo lolote la lufanywa mapinduzi ya kijeshi ilikuwa ni ishara ya hatari ya kutokea malumbano makali baina ya wafuasi wa nadharia ya kutenganisha kabisa dini na dola na wale wanaounga mkono Uturuki iwe zaidi nchi ya Kiislamu.

Uchaguzi mpya wa bunge utaipa Uturuki nafasi mpya. Mgawanyiko mpya wa nguvu za kisiasa sio kwamba utahakikisha kuchaguliwa bungeni kwa njia ya kidimokrasia rais wa 11 wa nchi hiyo. Lakini kwa sasa kidogo watu watapumua. Huenda sana chama chenye nguvu kabisa katika uchaguzi huo kikabakia kuwa kile cha Haki na Maendeleo cha waziri mkuu Tayyip Erdogan. Lakini huenda vyama vya Ki-Conservative na kile cha Social Democratic- vyama vya mirengo ya kulia, kushoto na katikati- vikakiuka hali zao za sasa za kusambaratika, hivyo kuweza kuchaguliwa na wananchi, na sio kuwa katika hali kama ilivyokuwa miaka mitano iliopita vilipopata chini ya thuluthi moja ya kura.

Pindi Tayyip Erdogan na chama chake cha AKP atarejea na wingi ule ule au mkubwa zaidi bungeni, basi itakuwa vigumu kuizuwia hali ya kuigeuza Uturuki kuwa dola ya Kiislamu zaidi. Hapo tena chama hicho, kikiwa na kura nyingi za wananchi, kitashikilia kwamba mtetezi wake achagukiwe kuwa rais wa nchi, mtetezi ambaye mke wake atakuwa anavaa mtandio. Na hapo tena kuna hatari ya demokrasia ya Uturuki kuzidi kuporomoka na kuwa ya daraja ya pili, kwani watu wasioelemea dini watazidi kulitaka jeshi lijiingize. Matokeo yake ni kwamba matarajio ya mbali ya Uturuki kuingizwa katika Umoja wa Ulaya yatafifia.

Miraji Othman