1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

uchaguzi nigeria

Admin.WagnerD9 Februari 2015

Serikali ya Nigeria imejikuta katika wakati mgumu baada ya uamuzi wake wa kuahirisha chaguzi za taifa hilo kwa kile ilichodai kuongezeka kwa mashambilizi ya kundi la Waisilamu wenye itikadi kali la Boko Haram.

https://p.dw.com/p/1EYCx
Nigeria Demonstration gegen Verschiebung der Wahl 7. Februar 2015
Waandamani wakipinga hatua ya kusogezwa mbele kwa uchaguzi wa Nigeria, muda mfupi kabla ya kutolewa kwa uamuziPicha: picture-alliance/AP Photo/O. Gbemiga

Kufuatia tatizo hilo upinzani umesema una lengo la kubinya demokrasia ya taifa hilo. Tume ya uchaguzi nchini Nigeria, mwishoni mwa juma ilitangaza uchaguzi wa rais na ule wa bunge utaahirishwa kutoka Februari 14 hadi Machi 28.

Uamuzi huu unatolewa baada ya wiki moja ya mashambulizi ya kundi la Boko Haram ya karibu kila siku, hasa katika maeneo ya kaskazini/mashariki ambako kumekuwa na kitisho cha kutofanyika uchaguzi kwa usalama.

Upinzani mkubwa kwa rais Jonathan

Lakini waangalizi wanasema changamoto ya upinzani anayopata rais wa sasa, Goodluck Jonathan, kutoka kwa mgombea wa upinzani kiongozi wa zamani wa kijeshi Muhammadu Buhari, imekuwa sababu kubwa ya kuchelewesha uhaguzi huo.

Nigerianischer Präsident Goodluck Jonathan 11.11.2014
Rais Goodluck Jonathan wa NigeriaPicha: picture-alliance/AP

Buhari amesema uhuru wa Tume Huru ya Uchaguzi INEC utakuwa umeingiliwa kwa kiasi kikubwa katika kipindi hiki cha wiki sita za nyiongeza. Aidha mgombea huyo ametoa wito kwa raia wa taifa hilo kuwa watulivu na kujiepusha na vurugu zozote, ambazo anadai zinasababishwa na chama tawala nchini humo PDP. Buhari amnekuliwa akisema "Tume ya huru ya uchaguzi INEC imefikia maamuzi mabaya. Mimi kama raia wa Nigera na mgombea kutoka upande wa upinzani, Naonesha kusikitishwa kwangu na kuvurugwa na uamuzi huu".

Tume ya uchaguzi haitokuwa huru

Katika mkutano wake wa waandishi habari mjini Abuja alisema pamoja na kwamba tume hiyo ya uchaguzi imeundwa kwa mujibu wa nguvu za kikatiba lakini kwa hivi sasa itakuwa kama imo kwenye kasha na itapaswa kutekeleta matakwa yake kwa shinikizo. "Napenda kutoa kauli madhubuti kabisa kwamba chama chetu hakiwezi kuvumilia kitendo chochote cha kuingiliwa zaidi mchakato wa uchaguzi. Ratiba mpya ya uchaguzi uliopangwa kufanyika Machi 28 na Aprili 11, mwaka 2015 lazima iwe takatifu". Alisema Buhari.

Wahlkampf in Nigeria 2015 Muhammadu Buhari
Muhammadu Buhari, mgombea wa upinzani NigeriaPicha: AFP/Getty Images/P. Utomi Ekpei

Mshauri wa masuala ya usalama wa Nigeria Sambo Dasuki alionya kuhusu usalama wa wapiga kura endapo uchaguzi ungefanyika Februari 14, kutoka na nguvu zote za kijeshi na usalama kuelekezwa katika operesheni kubwa dhidi ya Boko Haram.

Mataifa makubwa yaionya Nigeria

Marekani imesema imekatishwa tamaa kwa kiasi kikubwa na ucheleweshaji huo. Waziri wa Mambo ya Nje wa taifa hilo, John Kerry ameionya serikali ya Nigeria dhidi ya kutumia kigezo cha hali ya usalama kwa lengo la kubinya demokrasia. Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza Philip Hammod alitoa kauli kama hiyo.

Chama tawala cha rais Jonathan PDP kinakabiliwa na upinzani mkali kuwahi kutokea katika taifa hilo tangu kumalizika kwa utawala wa kijeshi mwaka 1999. Buhari, ambae anajinasibu kama kiranja wa kukabilina na tatizo sugu la ufisadi nchini humo, inaaminika kuwa na ushawishi mkubwa katika eneo lenye idadi kubwa ya Waislamu la Kaskazini, ambalo pia ndiko anakotokea.

Mwandishi: Sudi Mnette AFP/RTR
Mhariri:Yusuf Saumu