1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi wa Urais wa Timor Mashariki wakamilika kwa amani.

Omar Babu9 Aprili 2007

Uchaguzi wa urais wa Timor ya Mashariki uliofanyika leo unaelekea kuzidisha utata katika nchi hiyo huku wadadisi wa maswala ya kisiasa wakibashiri kwamba hapatakuwa na mshindi wa moja kwa moja. Nchi hiyo imekabiliwa na utata tangu mwaka mmoja uliopita ilipokumbwa na ghasia zilizotishia kuzuka vita vya wenyewe kwa wenyewe.

https://p.dw.com/p/CHGm
Rais wa Timor Mashariki anayeondoka, Xanana Gusmao.
Rais wa Timor Mashariki anayeondoka, Xanana Gusmao.Picha: AP

Waziri Mkuu, Jose Ramos-Horta, ambaye ni mshindi wa mwaka 1996 wa tuzo ya Nobel alipigiwa upatu kwamba angeibuka na ushindi wa moja kwa moja, lakini mambo yakawa kinyume.

Wagombea wanane ndio wanaochuana kwenye uchaguzi huo katika harakati ya kutaka kutwaa wadhifa wa urais ambao unashikiliwa na kiongozi wa zamani wa waasi, Xanana Gusmao.

Wachunguzi wamesema wapiga kura walijitokeza kwa wingi na kupiga kura kwa hali ya utulivu na amani.

Kulingana na wachunguzi hao, ni bayana kwamba kutakuwa na awamu ya pili ya uchaguzi katika nchi hiyo ambayo kabla ya uhuru wake ilitawaliwa na Indonesia kwa miongo mingi.

Kiasi watu laki tano na elfu ishirini na mbili wamejiandikisha kupiga kura katika nchi hiyo ambayo ina vituo zaidi ya mia saba vya kupiga kura.

Ulinzi mkali ulikuwa umeweka tangu asubuhi wapiga kura walipoanza kutunga foleni.

Hata hivyo kuna wasiwasi kwamba hali ya mambo haitatengemaa katika nchi hiyo inayokabiliwa na misukosuko ya kisiasa.

Mwanachama wa tume ya uchaguzi, Padre Martinho da Silva Gusmao anaelezea hofu aliyo nayo.

"Uchaguzi huu utabadilisha tu nyuso za wakuu wa serikali. Misukosuko itabaki pale pale. Hatuna mkakati wowote uliolengwa kurekebisha hali ya mambo kwa undani"

Ingawa wagombea wanane wanashiriki katika uchaguzi huo, wagombea watatu ndio wanaopigiwa upatu wa kutoa ngurumo za haja.

Orodha ya wagombea hao inaongozwa na Waziri Mkuu wa sasa, Jose Ramos-Horta.

Rais aliyeko madarakani, Xanana Gusmao, ameamua kutotetea wadhifa wake, na badala yake kusubiri uchaguzi wa bunge utakaofanyika miezi michache ijayo ili ajitose kuwania wadhifa wa Waziri Mkuu.

Jose Ramos-Horta, anayetarajiwa na wengi kushinda awali, alielezea alikuwa na imani kwamba shughuli nzima hiyo ya uchaguzi ingefana.

Mara baada ya kupata uhuru wake mwaka 2002, Timor Mashariki ilipata sifa kemkem kutokana na ari na kujitolea kwake katika ujenzi wa taifa.

Mwaka uliopita ghasia zilitibuka baada ya hatua ya aliyekuwa Waziri Mkuu, Mari Alkatiri, kuwatimua wanajeshi kadhaa.

Hatua hiyo ya waziri mkuu ilisababisha vita kati ya wanajeshi mahasimu na pia ghasia za magenge , uporaji na ukosefu wa utangamano kwa jumla.