1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ufumbuzi wa mzozo wa madeni Ulaya

Riegert,Bernd/ZPR-P.Martin/RTRE30 Januari 2012

Takriban viongozi wote wa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya wanatazamiwa kuidhinisha mkataba mpya wa kuimarisha ushirikiano wa kifedha watakapokutana leo mchana mjini Brussels, Ubeligiji.

https://p.dw.com/p/13sri
Umoja wa Ulaya watafuta ufumbuzi wa tatizo la madeniPicha: dapd

Lengo ni kupata suluhisho la kudumu kuhusu mzozo wa madeni katika kanda ya euro. Bado kuna masuala madogo ya kujadiliwa lakini Ujerumani inaamini kuwa mambo yatakwenda vizuri. Na hiyo wala haishangazi kwani fikra ya kuziwajibisha nchi wanachama kuwa na udhibiti mkali zaidi wa bajeti, imetoka kwa Kansela wa Ujerumani Angela Merkel.

Mkutano wa leo wa viongozi wa Umoja wa Ulaya ni wa 17 kufanyika katika kipindi cha miaka miwili iliyopita katika jitahada ya kuyamaliza matatizo ya madeni serikalini. Kipaumbele ni kuongeza nafasi za ajira na kuimarisha ukuaji wa kiuchumi. Vile vile, watashughulikia mfumo wa kisheria kuhusiana na mfuko wa kuziokoa nchi zilizo na madeni katika kanda ya euro. Kwenye mkutano wa Desemba mwaka jana, Kansela Merkel alitangaza kwa furaha kubwa kuwa hatua muhimu imechukuliwa kuelekea kwenye suluhisho la kudumu.

Wakati huo huo, rais wa Benki Kuu ya Ujerumani Jens Weidmann amesema, mkataba huo ni sehemu muhimu ya ufumbuzi wa mzozo wa madeni lakini kwa maoni yake, mkataba huo pekee, hautosaidia kuumaliza mzozo wa madeni. Kuambatana na mkataba huo mpya,serikali zitawajibishwa kupunguza nakisi katika bajeti - yaani kukomesha kabisa mtindo wa kuzidisha madeni serikalini.

Mkataba huo mpya hauhusiki na mkataba halisi, kwani Uingereza imetumia kura ya turufu kuyapinga makubaliano hayo mapya. Waziri mkuu wa Uingereza David Cameron ana hofu kuwa nchi zitakazotia saini mkataba huo mpya hazitokuwa na usemi katika masuala yanayohusika na bajeti zao. Lakini Kansela wa Ujerumani anakanusha tuhuma kuwa Ujerumani yenye uchumi mkubwa kabisa katika kanda ya euro inataka kutumia ushawishi wake. Amesema.

"Hakuna nchi yo yote inayoweza kuipatia mafunzo upande huo nchi nyingine. Lakini ni dhahiri kuwa tunapaswa kujadiliana. Na hatuwezi kukodoa macho tu na kusema, kila mmoja atafanya apasavyo tu. Tuko tayari pia kujifunza kutoka kwa wenzetu. Sio la ukubwa hata kidogo."

Weltwirtschaftsforum Davos Bundeskanzlerin Angela Merkel
Kansela wa Ujerumani Angela MerkelPicha: AP

Kwa kweli, kanuni za mkataba unaolenga kuimarisha umoja katika masuala ya fedha, sio mpya hivyo, isipokuwa kwa kanuni za kudhibiti madeni. Katika siku zijazo, nchi wanachama watakaotia saini mkataba huo mpya ndio watakaopatiwa msaada kutoka mfuko wa kuziokoa nchi za kanda ya euro inayojumuisha nchi 17. Baada ya kuidhinishwa na mabunge ya nchi zilizotia saini, mkataba huo unatazamiwa kuanza kufanya kazi katika kipindi cha mwaka mmoja ujao. Wataalamu wanakubaliana kuwa mkataba huo mpya hautosuluhisha mzozo wa hivi sasa lakini mafanikio yake yatadhihirka katika siku zinazokuja.