1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Afrika kuijadili Cote d'Ivoire

Halima Nyanza10 Machi 2011

Rais wa Cote d'Ivoire anayetambuliwa kimataifa Alassane Ouatarra leo anahudhuria mkutano wa Umoja wa Afrika, baada ya kuondoka jana mjini Abidjan ikiwa ni mara ya kwanza kutoka nje ya nchi hiyo, baada ya uchaguzi.

https://p.dw.com/p/10WpX
Viongozi wanaobishania madaraka Cote d'voire Laurent Gbagbo na Alassane OuattaraPicha: AP/DW

Mkutano huo wa Umoja wa Afrika pia unatarajiwa kupata suluhisho la mzozo huko Cote d´Ivoire, ambako Laurent Gbagbo anayeng'ang'ania madarakani.

Mkutano wa leo wa viongozi wa Umoja wa Afrika, utakaofanyika katika mji mkuu wa Ethiopia Addis Ababa, unafanyika kutokana na kuongezeka kwa ghasia zilizosababishwa na mabishano ya viongozi hao wawili ya nafasi ya uongozi, ambazo zimesababisha kuuawa kwa watu zaidi, maelfu kuwa wakimbizi na hatari ya kuzuka kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Akizungumzia mkutano huo, msemaji wa Ouattara Anne Ouloto amesema wanatarajia uthibitisho wa kutambuliwa kwa Ouattara kama mshindi wa uchaguzi wa rais na msimamo utakaowezesha Laurent Gbagbo kuondoka madarakani.

Gbagbo amepuuzia mwaliko wa Umoja wa Afrika kuhudhuria mkutano huo na marais watano wa Afrika walio na jukumu la kuupatia ufumbuzi mzozo huo wa kisiasa na badala yake ametuma mwakilishi.

Wakati huohuo, msaidizi wa Bwana Gbagbo Laurent Dona-Fologo amesema hakuna cha kujadiliwa kuhusiana na matokeo ya uchaguzi wa rais nchini humo, uliofanyika Novemba 28 mwaka jana.

Lakini katika hatua nyingine chama cha Bwana Gbagbo kimearifu kuwa hajakwenda nchini Ethiopia kutokana na kuzorota kwa hali ya usalama nchini mwake, wakati ambao wafuasi wake wamekuwa wakidai kuwa mkutano huo ni mtego wa kumuondoa nje ya nchi.

Viongozi watano wa nchi za Kiafrika, walio na kazi ya kuupatia ufumbuzi mzozo huo wa kisiasa nchini Cote d'Ivoire, walikutana jana mjini Addis Ababa kujadili kwa kina mapendekezo, ambayo watayawasilisha katika mkutano wa leo.

Marais hao ni Jacob Zuma wa Afrika kusini, Jakaya Kikwete wa Tanzania, Idriss Deby wa Chad, Mohamed Ould Abdel Aziz wa Mauritania na Blaise Compaore wa Burkina Fasso.

Wakati ambapo mpinzani wake akiwa ametoka kwa mara ya kwanza kuhudhuria mkutano wa Umoja wa Afrika, Rais Gbagbo amepiga marufuku ndege za Umoja wa Mataifa na zile za jeshi la Ufaransa kupita juu ya anga na kutua nchini humo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotangazwa kupitia televisheni ya nchi hiyo imesema ndege zinazopita kwa dharura au kutua ni lazima kwanza kupata kibali cha wizara inayoshughulika na usafiri nchini humo.

Wakati huohuo, Rais Barack Obama wa marekani amelaani kile alichokiita ''ghasia zilizojaa chuki'' nchini Cote d'Ivoire na kusema kuwa Marekani imesikitishwa na mapigano yanayoendelea, ambayo yamesababisha vifo vya raia kadhaa.

Ameelezea kushtushwa kwake na mauaji ya raia wakati wa maandamano ya amani, ambayo wengi wake walikuwa wanawake.

Mwandishi: Halima Nyanza(afp)

Mhariri:Aboubakary Liongo