1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Afrika na umoja wa mataifa zashutumu shambulio mjini Mogadishu

Sekione Kitojo4 Desemba 2009

Katibu mkuu wa umoja wa mataifa na rais wa halmashauri ya umoja wa Afrika wameshutumu shambulio la kujitoa muhanga mjini Mogadishu lililosababisha watu 19 kuuwawa jana Alhamis.

https://p.dw.com/p/Kq8i
Mwanajeshi wa jeshi la serikali ya Somalia akifanya doria katika moja kati ya mitaa ya mjini Mogadishu nchini Somali.Picha: AP

Umoja wa Afrika umeshutumu vikali shambulio la bomu la kujitoa muhanga ambalo limeuwa watu 19, ikiwa ni pamoja na mawaziri watatu wa serikali ya mpito nchini Somalia. Wakati huo huo msemaji wa kundi kubwa la waasi nchini Somalia la al Shabaab amekana leo kuwa kundi hilo linahusika na shambulio hilo.

Rais wa halmashauri ya umoja wa Afrika Jean Ping ameshutumu vikali shambulio hilo lililotokea jana Alhamis. Kitendo hicho cha kinyama ambacho kinalenga katika kuharibu utaratibu wa kuleta amani hakitazuwia umoja wa Afrika kutoa msaada kwa serikali ya mpito ya Somalia kuleta hali ya maridhiano nchini humo, imesema taarifa iliyotolewa na ofisi ya rais wa halmashauri hiyo .

Wakati huo huo katibu mkuu wa umoja wa mataifa Ban Ki-moon na baraza la usalama la umoja wa mataifa limeshutumu vikali shambulio hilo.

UN-Generalsekretär Ban Ki-Moon spricht auf der UN-Welternährungskonferenz in Rom, Italien
Katibu mkuu wa umoja wa mataifa Ban Ki-moon , ameshutumu vikali shambulio la kujitoa muhanga nchini Somalia.Picha: AP

Katibu mkuu amesema kuwa shambulio hilo litaimarisha tu nia ya serikali ya Somalia na watu pamoja na washirika wengine kuendelea na juhudi zao za kupambana na ugaidi nchini Somalia. Hili amesema katibu mkuu Ban Ki-moon kuwa ni shambulio la kihalifu dhidi ya watu ambao wanania ya kuleta maendeleo kwa njia ya amani.

Serikali ya Somalia inayoungwa mkono na umoja wa mataifa ya rais Sheikh Sharif Ahmed inadhibiti mitaa michache tu ya mji mkuu Mogadishu. Siku chache kabla ya shambulio la jana Alhamis , wakaazi wamesema kuwa serikali ilikuwa inapanga shambulio jipya dhidi ya waasi.

Mkaazi mmoja wa mjini Mogadishu Badra Yussuf Ali hata hivyo amesema kuwa jamii imeingiwa na hofu kubwa kutokana na shambulio hilo la kujitoa muhanga.

Hali kwa sasa iko shwari na hata hoteli palipotokea shambulio hilo ni shwari. Watu bado wana majonzi baada ya shambulio hilo na kuna hali ya taharuki katika jamii.

Waziri wa afya wa Somalia Qamar Aden Ali, waziri wa elimu Ahmed Abdulahi Waayeel na waziri wa elimu wa juu Ibrahim Hassan Addow wameuwawa katika shambulio hilo. Waziri wa michezo Saleban Olad Roble amejeruhiwa na yuko katika hali mbaya.

Wakati huo huo msemaji wa kundi la wapiganaji wa al- Shabaab amekana leo kuwa kundi hilo limehusika katika shambulio hilo la hapo jana. Wanafunzi pamoja na wazazi wao ni miongoni mwa watu waliouwawa katika shambulio hilo. Msemaji wa Al-Shabaab Sheikh Ali Mohammed Rage amewaambia waandishi habari kuwa kundi hilo halikuhusika na shambulio hilo. Amesema kuwa kundi hilo linaamini kuwa huenda na njama iliyofanywa na serikali yenyewe. Ameongeza Rage kuwa hiyo si katika utaratibu wa kundi la al Shabaab kushambulia watu wasio na hatia. Rage amesema kuwa mgawanyiko mkubwa wa kisiasa umejitokeza kati ya viongozi wa juu wa serikali katika serikali ya rais Sheikh Sharif Ahmed mjini Mogadishu. Amedokeza kuwa tunafahamu baadhi ya maafisa wa serikali waliondoka katika eneo hilo dakika chache kabla ya shambulio. Na hii inaonyesha kuwa wanahusika na shambulio hilo.

Mwandishi : Sekione Kitojo / AFPE / RTRE

Mohammed Abdul Rahman