1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya wazungumzia kutumwa wanajeshi Tchad na Afrika kati

Oummilkheir28 Septemba 2007

Mawaziri wa ulinzi wa mataifa 27 wanachama wa Umoja wa Ulaya wanakutana kuanzia leo mjini Evora Ureno,kuzungumzia mustakbal wa Kosovo na uhusiano pamoja na bara la Afrika.

https://p.dw.com/p/CH7V
Wakimbizi wa Darfur
Wakimbizi wa DarfurPicha: AP

Ufaransa inapanga kuwatanabahisha washirika wake wakubali kuchangia wanajeshi katika kikosi cha Umoja wa Ulaya,watakaopelekwa Tchad na katika jamhuri ya Afrika kati kama ilivyoamuliwa na Umoja wa mataifa.

Katika mkutano huo wa siku mbili katika mji wa EVORA,umbali wa kilomita mia moja mashariki ya mji mkuu wa ureno Lisbon,mawaziri 27 wa ulinzi wa Umoja wa ulaya wanatazamiwa kuzungumzia opereshini za kijeshi za Umoja wa ulaya zinazoendelea nchini Bosnia pamoja na zile zinazotazamiwa kuanzishwa Tchad na jamhuri ya Afrika kati, kwa ushirikiano pamoja na Umoja wa mataifa.

Mada hii ya pili itajadiliwa pia kesho katika kikao maalum kuhusu Afrika-kipa umbele cha wadhifa wa Ureno-mwenyekiti wa zamu wa Umoja wa Ulaya.

Jumanne iliyopita ,baraza la usalama la Umoja wa mataifa,liliidhinisha shughuli za wanajeshi wa umoja wa ulaya ili kurahisisha kurejea nyumbani malaki ya watu walioyapa kisogo mapigano ya wenyewe kwa wenyewe katika jimbo la Darfour linalopakana na Tchad na jamhuri ya Afrika kati-kwa kushirikiana na askari polisi 300 wa Umoja wa mataifa watakaopelekwa kuwasaidia polisi wa nchi hizo mbili husika.

Watakua na jukumu la kuwalinda wanajeshi 26 elfu wa kikosi cha pamoja cha Umoja wa mataifa na umoja wa Afrika watakaowekwa hatua baada ya hatua Darfour hadi ifikapo kati kati ya mwaka 2008.

Umoja wa ulaya unadhamiria kuchangia jumla ya wanajeshi elfu nne. Ufaransa,itakayoongoza kikosi hicho inapanga kuchangia zaidi ya nusu wanajeshi hao.

Wanadiplomasia wanaamini wanajeshi elfu kadhaa wa Ufaransa hawatotokea kwenye kikosi cha nchi hiyo kilichoko tangu miaka kadhaa nchini Tchad .

Hali hiyo inaweza kuzituliza baadhi ya nchi za Ulaya zinazohofia tume ya wanajeshi wa umoja wa ulaya isije ikajumuishwa na wanajeshi wa ufaransa waliowekwa Tchad kufuatia makubaliano ya pande mbili kati ya Paris na Ndjamena.

Kishindo chengine kinachoukabili mkutano huo wa siku mbili wa Evora ni ile hali kwamba Umoja huo wa Ulaya ambao wanachama wake 21 kati ya 27 ni wanachama pia wa jumuia ya kujihami ya magharibi NATO,unashindwa kupata wanajeshi kutokana na majukumu chungu nzima yanayosimamiwa na NATO,naiwe nchini Afghanistan na Kosovo,Umoja wa Ulaya huko Bosnia au Umoja wa mataifa nchini Libnan.

Ujerumani imeshasema haijaweza kujiunga na kikosi cha umoja wa ulaya kwa bara la Afrika kutokana na kuwajibika kwake katika sehemu nyengine za dunia.

Kwa upande mwengine lakini Sweeden inasemekana iko tayari kuchangia wanajeshi mia kadhaa.

Hata hivyo haifikiriwi kama uamuzi wa nchi gani itachangia wanajeshi wangapi ,utapitishwa mwishoni mwa mkutano huu wa Evora hapo kesho.