1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ureno yaomba Msaada wa Fedha

Martin,Prema7 Aprili 2011

Baada ya kusita muda mrefu, Ureno sasa imeamua kuomba msaada wa fedha kutoka Umoja wa Ulaya, ili kuhakikisha usalama wa uchumi wake.

https://p.dw.com/p/RG6E
Portugal's Prime Minister Jose Socrates makes an address, Wednesday, April 6 2011, in Lisbon. Portugal's prime minister says his country will ask for a bailout due to its high debts and difficulty raising money on international markets. Prime Minister Jose Socrates said Wednesday "the government decided today to ask the European Commission for financial help." (AP Photo/Jose Sena Goulao, Pool)
Waziri Mkuu wa mpito wa Ureno, Jose SocratesPicha: AP

Haijulikani iwapo nchi hiyo itachukua mkopo wa kujishikilia kwa muda au itahitaji msaada maalum ulioanzishwa kwa lengo la kulinda thamani ya sarafu ya Euro. Hata hivyo Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Jose Manuel Barroso amesema, ombi la Ureno litashughulikiwa na umoja huo, haraka iwezekanavyo. Sasa, masoko ya fedha nchini Ureno yanaweza kupumua kidogo, baada ya serikali ya mpito nchini humo, kubadili msimamo wake na kuamua kuomba msaada wa fedha. Kwa hivyo Ureno inafuata nyayo za Ugiriki na Ireland zilizotangulia kuomba msaada wa fedha baada ya kukabiliwa na matatizo makubwa ya deni. Wataalamu wa uchumi wanasema, serikali ya Ureno hapo awali haikutaka kukiri hali halisi ya kiuchumi ilipokuwa ikisita. Hiyo jana waziri mkuu wa mpito Jose Socrates alipotangaza kuwa Ureno sasa itaomba msaada huo wa fedha alieleza hivi:

"Benki na makampuni ya Ureno yameshuhudia viwango vya uwezo wa kupata mikopo, vikiporomoka kwa kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa. Kwa hivyo, Ureno haina budi kuomba msaada wa fedha, ili kusaidia benki na uchumi kwa jumla. "

Wakati wa kuomba msaada umewadia

Socrates amesema amejaribu kila njia lakini sasa umewadia wakati wa kuamua kuchukua mkopo ili kuunusuru uchumi wa nchi. Mpango wa serikali wa kutaka kupunguza matumizi yake ulishindwa kuungwa mkono katika kura ya imani iliyopigwa bungeni na serikali ikajiuzulu tarehe 23 Machi. Wasiwasi kuhusu uchumi wa Ureno, umesababisha nchi hiyo kushushwa katika orodha inayotolewa na mashirika yanayotathmini uwezo wa taifa kulipa madeni. Uamuzi wa hiyo jana umesaidia pia kupunguza wasiwasi katika nchi za Ulaya zinazotumia sarafu ya Euro.

Portuguese Finance Minister Fernando Teixeira dos Santos, standing center, answers members of parliament during the debate of his minority government's latest austerity package Wednesday, March 23 2011, at the Portuguese parliament in Lisbon. If lawmakers fail to back the package the governmanet could fall puting Lisbon into political limbo just as it faces huge debt repayment deadlines and desperately needs markets' confidence. (AP Photo/Armando Franca)
Bunge la Ureno mjini LisbonPicha: AP

Waziri mkuu wa mpito Socrates, hakutaja kiwango cha msaada unaohitajiwa, lakini afisa mmoja kutoka kanda ya Euro ametathmini kuwa katika kipindi cha miaka mitatu ijayo, Ureno huenda ikahitaji mkopo wa Euro bilioni 60 hadi 80 kutoka Umoja wa Ulaya na Shirika la Fedha la Kimataifa IMF. Lakini Ureno itapaswa kukubali masharti magumu ya kupunguza matumizi yake ili iweze kusaidiwa. Masharti hayo huenda yakawa magumu kuliko yale ya Ugiriki na Ireland.

Serikali ya mpito ya Ureno imesema, haina madaraka makubwa na bunge limevunjwa mpaka uchaguzi uliopangwa kufanywa tarehe 5 mwezi wa Juni. Na kawaida linahitajiwa kuidhinisha makubaliano kabla ya kupata mkopo. Kiongozi wa chama kikuu cha upinzani Social Democrats amesema yeye anaunga mkono ombi la msaada. Lakini chama hicho kwa kupinga mpango wa kupunguza matumizi uliopendekezwa bungeni mwezi uliopita, kilichochea mzozo ulioibuka.