1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi kuondowa vikosi vyake kutoka Georgia leo

Mohamed Dahman18 Agosti 2008

Urusi imetangaza kwamba itaanza kundowa vikosi vyake kutoka Georgia leo hii baada ya vita ambavyo vimeleta madhara makubwa kwa taifa hilo la Bahari Nyeusi na kuzusha hofu ya usambazaji wa nishati kwa Bara la Ulaya.

https://p.dw.com/p/F091
Rais Mikhail Saakashvili wa Georgia akizungumza na Kansela Angela Merkel wa Ujerumani wakati walipokutana katika mji mkuu wa Georgia Tbilisi, Jumapili ya tarhe 17 Augusti 2008.Picha: AP

Rais Mikheil Saakashvili wa Georgia ambaye uvamizi wake ulioshindwa kwa jimbo lililojitenga linaloungwa mkono na Urusi la Ossetia Kusini kumepelekea kujibu mapigo makali kutoka Urusi kulikoishtuwa dunia ametowa wito kwa waangalizi wa kimataifa kuangalia kuondolewa huko kwa vikosi vya Urusi kutoka Georgia.

Ameuambia mkutano wa waandishi wa habari akiwa pamoja na Kansela Angela Merkel wa Ujerumani mjini Tblisi nchini Georgia hapo jana kwamba dunia inapaswa kuangalia.

Amesema wanahitaji wayakinisho kuondolewa kwa vikosi hivyo yumkini na waangalizi wa Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya Usalama na Ushirikiano na msaaada wa kibinaadamu kuwafikia kila mtu na mwishowe wanajeshi wa kulinda amani kukalia maeneo ya mzozo na kutafuta ufumbuzi wa dhati wa mzozo huo kwa maslahi ya makundi yote ya kikabila.

Kadhalika amerudia haki ya kujitawala kwa nchi yake.

Georgia haitoachilia kilomita yoyote ile ya mraba ya ardhi yake.Na kitokee chochote kile katu hatotukubaliana na ukweli wa kutwaliwa kwa ardhi yetu au kuzitenganisha baadhi ya ardhi zetu kutoka Georgia kwa jaribio la kuhalalisha utokomezaji wa kizazi.

Akizungumza katika mkutano huo wa pamoja na waandishi wa habari mjini Tblisi Kansela Angela Merkel wa Ujerumani ameshinikiza kuheshimiwa kwa makubaliano ya hivi karibuni ya kusitisha mapigano yaliotiwa saini na Rais Dmitry Medvedev wa Urusi hapo Jumamosi siku moja baada ya kutiwa saini na Rais Saakashvili wa Georgia.

Merkel pia amesisitiza kwmba mchakato huo haupaswi kuzoroteshwa.

Merkel pia amerudia tena msimamo wa Ujerumani kwamba suala la kuheshimiwa kwa mipaka ya Georgia halina mjadala na kwamba mipaka yake hiyo haipaswi kukiukwa.

Kiongozi huyo wa Ujerumani matamshi yake yanaweza kuikasirisha Urusi kwa kusema kwamba kuna matarajio ya Georgia kuwa mwanachama wa Jumuiya ya Kujihami ya Mataifa ya Magharibi NATO kwamba kila nchi huru kwa pamoja zinaweza kulijadili suala hilo katika mkutano wa mwezi wa Desemba.

Rais Dmitry Medvedev akitangaza kuondolewa kwa vikosi vya Urusi kutoka Georgia leo hii wakati wa mazungumzo yake ya simu na Rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa hakutowa muda wa mwisho wa kuondolewa kwa vikosi hivyo.

Urusi imeweka wazi kwamba haioni matumaini kwa kipindi cha usoni Ossetia Kusini kuunganishwa na Georgia.