1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Utafiti wasema Bara la Afrika linaweza kujitegemea.

2 Desemba 2010

Mabadiliko ya hali ya hewa ni pigo kwa maendeleo Afrika.

https://p.dw.com/p/QOMA
Mfumo wa kutegemea misaada ya chakula barani Afrika unaweza kubadilishwa.Picha: picture alliance/chromorange

Mataifa ya Afrika yanaweza kusitisha mfumo wa kutegemea chakula kutoka nje na yaweze kuzalisha chakula cha kutosha kukidhi mahitaji ya idadi ya watu inayoongezeka katika kipindi cha kizazi kimoja licha ya changamoto za mabadiliko ya tabia nchi. Haya ni kwa mujibu wa utafiti uliotolewa katika mkutano unaoendelea kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa mjini Cancun, Mexico.

Utafiti huo unadokeza kwamba mimea itakayostahimili joto jingi, kiangazi au mafuriko, mikakati ya kuwasaidia wakulima wadogo wadogo na kuhusika zaidi kwa viongozi katika kutunga sera juu ya kuimarishwa kwa miundo mbinu kuanzia usafiri ha di elimu, ndiko kunahitajika ili lengo hilo liafikiwe.

Profesa Calistous Juma wa chuo kikuu cha Harvard ndiye aliongoza utafiti huo na amesema bara la Afrika linaweza kujilisha na kubadilisha mtazamo uliopo wa kuagizia chakula na kujitegemea katika kizazi kimoja.

Utafiti huo unaonyesha kwamba asilimia 70 ya Waafrika wanahusika na kilimo lakini kiasi ya watu milioni 250 au robo ya idadi ya watu katika bara hilo hawapati lishe bora. Idadi hiyo imeongezeka kwa watu milioni 100 tangu mwaka wa 1990.

29.11.2010 DW-TV Global 3000 klima marokko 3
Utafiti wa Havard unasisitiza kuwa sera bora ni msingi wa kujitegemea.Picha: DW-TV

Profesa Juma wa kitengo kinachoshughulikia maendeleo ya kimataifa katika chuo kikuu cha Harvard, aliliambia shirika la habari la Reuters kwamba kujitegemea kwa bara la Afrika kutahitaji mabadiliko makubwa katika utungaji sera zitakazositisha misaada ya chakula kutoka nje.

Hata hivyo Profesa Juma alisisitiza kwamba tatizo la mabadiliko ya tabia nchi linavuruga mkakati huo. Utafiti huo umetolewa huku mkutano kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa ukiendelea mjini Cancun, Mexico.

Jopo la wanasayansi kutoka Umoja wa Mataifa wamesema hadi watu milioni 220 barani Afrika wanaweza kukosa maji ifikapo mwaka wa 2020 kutokana na kiwango kinachoongezeka cha joto, mafuriko, maporomoko ya ardhi, kiangazi na kuongezeka kwa majangwa.

Utafiti huo uitwao ‘mavuno mapya, uvumbuzi katika sekta ya kilimo barani Afrika’ unatoa mwito kwa viongozi wa kitaifa washiriki zaidi katika kusuluhisha matatizo ya maji, nishati, usafiri, mawasiliano na elimu.

Unadhihirisha kuwa ni muhimu mimea itakayostahimili changamoto za hali ya hewa izinduliwe ili kuwa na uhakika wa kupata chakula. Rais wa Costa Rica, Laura Chincilla ameupigia upatu utafiti huo kuhusu mustakabali wa uwepo wa chakula barani Afrika, akisema huenda manufaa yatakayoafikiwa yatayanufaisha mataifa mengine hasa kusini mwa Marekani.

Mwandishi: Peter Moss /Reuters

Mhariri: Abdul-Rahman