1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uturuki na Umoja wa Ulaya

20 Januari 2009

Umoja wa Ulaya uiambie ukweli Uturuki ?

https://p.dw.com/p/GclJ
Erdogan-waziri mkuu (Uturuki)Picha: AP

Je, mazungumzo ya uwanachama wa Uturuki katika Umoja wa Ulaya ni kiini macho tu ? Inaonekana kana kwamba, uanachama huo ni jambo lisilolingana na ukweli wa hali ya mambo.Kwani, msimamo wa hadi sasa uliochukuliwa na Umoja wa Ulaya wa ngoja-ngoja na hata wa kuikomea mlango Uturuki ni dhahiri kabisa.

Waziri mkuu Erdogan wa Uturuki adhihirika amefadhahishwa mno.Katika kutimiza masharti yanayotakiwa ili nchi yake ipewe uanachama wa Umoja wa Ulaya, aweza kutoa ushahidi wa mageuzi mengi iliotakiwa Uturuki kuyafanya.

Kutokana na mvutano wa gesi ulioibuka kati ya Urusi na Ukraine, Uturuki sasa kutumiwa kama kituo cha kupita kusafirishia gesi, imekuwa muhimu zaidi kimkakati wa kisiasa.Je, karata hiyo bado haitoshi kuifungulia mlango Uturuki kujipatia uanachama kamili ?

Rasmi, Uturuki imeshapita njia hiyo na majadiliano ya kujiunga na Umoja wa Ulaya yanaendelea ,tena kutoka sahifa moja hadi nyengine na kama inavyosemekana katika Umoja wa Ulaya ,yanashughulikiwa ingawa pole pole ,lakini yanashughulikiwa.

Erdogan na wananchi wengi wa Uturuki wanahisi Umoja wa Ulaya hauikaribishi Uturuki. Baadhi ya viongozi, mfano wa Kanzela Angela Merkel wa Ujerumani, wanasema wazi kuwa hawataki. Lakini, pale Rais wa Tume ya Umoja wa Ulaya, Jose Manuel Barroso, akitoa ahadi,inapasa kuushawishi umma barani Ulaya kuukubali uanachama wa Uturuki, basi hakuna tofauti .

Kwani, wingi wa wakaazi wana shaka shaka na wengine hawataki kabisa na hakuna kinachobainisha badiliko la nia.Sio tu mageuzi ambayo bado Uturuki haijayatekeleza au juu ya uhusiano wake na mwanachama wa Umoja wa Ulaya- kisiwa cha Cyprus. kizuwizi, kimsingi, kinakwenda mbali zaidi:

Watu wengi katika nchi za asili za Umoja wa Ulaya wana dhana kuwa Umoja wa Ulaya pale ulipopanuliwa kuingiza wanachama zaidi 9 hapo 2004 ulikuwa tayari umesheheni. Wakati huo huo haukufanya mageuzi yake ya ndani ili kuuwezesha kutenda au kujistawisha.

Hata kielezo hiki hakisemi yote: Kuna zaidi hisia kwamba Uturuki, kimila na kitamaduni, hailingani na Ulaya. Upinzani mkubwa unashikamana na kuwa Uturuki ni nchi ya kiislamu yenye athari zake tangu za kisiasa hata za kimila. Lakini Uturuki ingekuwa nchi ndogo, hali ya mambo ingelikuwa vyengine kabisa.

Uturuki hivi sasa ina wakaazi milioni 70 na kwa vile wakaazi wake wengi ni vijana, hautapita muda itaipita Ujerumani kwa idadi ya wakaazi. Uturuki ikiwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya itakuwa na wakaazi wengi zaidi na hivyo itaongeza uzito wake katika sera za Umoja wa Ulaya na hivyo kuzishawishi mno.Nani anaweza kuhakikisha kuwa Uturuki itabakia dola lisiloelemea dini ?

Tayari hivi sasa kuna mitindo wazi ya kuelemea Uislamu wenye itikadi kali.Ishara zote zinaelekeza kuwa na usuhuba wa karibu zaidi baina ya Umoja wa Ulaya na Uturuki na sio uwanachama kamili.

Kubadilisha msimamo huu bila ya ridhaa ya wananchi wa Ulaya,sio tu hakuingii maanani, bali pia ni hatari. Hatahivyo, wanasiasa wengi zaidi wa Umoja wa Ulaya wangepaswa kuonesha ujasiri katika kuiambia ukweli huo Uturuki, kwani hakuna kibaya zaidi kama kuendesha mazungumzo ya kiini macho, tena kwa muda wa muongo mzima.