1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa Afrika kushirikiana ili kupambana na ugaidi

23 Aprili 2024

Viongozi wa nchi za Afrika wamekutana mjini Abuja nchini Nigeria katika mkutano wa kilele wa kukabiliana na ugaidi, hivyo kutoa wito wa kuwepo ushirikiano zaidi wa kikanda ili kukabiliana na tatizo hilo.

https://p.dw.com/p/4f4Sn
Mkutano wa ECOWAS mjini  Abuja
Viongozi wa Kiafrika katika Mkutano wa Jumuiya ya ECOWAS mjini Abuja, NigeriaPicha: Kola Sulaimon/AFP/Getty Images

 Katika mkutano huo,viongozi hao walijadiliana kuhusu changamoto za kiusalama barani humo na kutafuta suluhu za kukabiliana na ugaidi, na moja wapo ikiwa ni kuunda jeshi la kikanda.

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina Mohammed aliuambia mkutano huo kuwa kitovu cha ugaidi kimehama kutoka eneo la Mashariki ya Kati na Kaskazini mwa Afrika hadi maeneo ya Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Soma pia: Tishio la ugaidi ni kubwa katika eneo la migogoro la Afrika

Wanamgambo wenye itikadi kali za Kiislamu wamejiimarisha katika eneo la Sahel kuanzia nchini Mali, na kutanua udhibiti wao maeneo ya kusini na hivyo kuyatishia mataifa ya pwani ya Afrika Magharibi, Pembe ya Afrika, Ziwa Chad na hata Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.