1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa G8 wamesema Gaddafi lazima ajiuzulu

27 Mei 2011

Viongozi wa kundi la mataifa ya G8 watoa kauli kali dhidi ya kiongozi wa Libya anayeripotiwa amepoteza imani kwa wananchi anaowaongoza kwa hivyo lazima ajiuzulu.

https://p.dw.com/p/11P7p
Viongozi wa G8 wakiwa nchini UfaransaPicha: AP

Taasisi za fedha za kimataifa zikiahidi kutoa kiasi cha dola bilioni 20 za kimarekani kwa ajili ya kufanikisha mchakato wa kuimarisha demokrasia katika nchi za Misri na Tunisia.

Mkutano huo wa kundi la mataifa tajiri kiviwanda duniani ya G8 unatarajiwa kumalizika leo katika mji wa kitalii wa Deauville, Ufaransa.

Majadiliano kuhusu mada mbalimbali yanaendelea lakini haijawa wazi kama kutatolewa kauli kali kuhusu Urusi ambayo imechukua msimamo tofauti katika kutafuta ufumbuzi wa mgogoro wa Libya.

Katika tamko hilo la nchi za G8 limesema ni wazi kwamba Gaddafi na utawala wake, ameendelea kufanya uovu dhidi ya raia wa nchi hiyo kwa hivyo uhalifu huo hauwezi kuachwa.

'Naye Rais Barack Obama wa Marekani, amesema nchi yake na Ufaransa watashirikiana bega kwa bega na Jumuiya ya Kujihami ya NATO mpaka ipatikane suluhu nchini Libya.

G8 Gipfel in Deauville Frankreich
Rais Barack Obama na Rais Nicolas Sarkozy wa UfaransaPicha: dapd

Rais huyo amesema wamekubaliana kwamba kuna hatua imepigwa katika utekekelezaji wa kampeni hiyo.

" Tumekubali kwamba tumepiga hatua katika kampeni yetu, lakini matakwa ya azimio la Baraza la Usalama la Umoja Mataifa kuwalinda raia haliwezi kutimia wakati Gaddafi akiendelea kuwemo nchini Libya, akielekeza vikosi vyake kufanya ukandamizaji dhidi ya wa watu wa Libya" alisema Obama

Obama ambaye alikuwa anazungumza muda mfupi baada ya mkutano wake na rais Nicolas Sarkoz wa Ufaransa alisema wamejipanga kumaliza kazi hiyo.

Mkutano huo wa siku mbili wa kundi la mataifa tajiri yalioendelea kiviwanda G8 umeunga mkono jitihada za kuchachua demokrasia mpya katika nchi za kiarabu.

Taasisi za fedha za kimataifa zitatoa kiasi cha dola za kimarekani bilioni 20 kufanikisha upatikanaji wa amani nchini Tunisia na Misri.

Fedha hizo zitakazosimamiwa na Shirika la Fedha la kimataifa, IMF, Benki ya Vitega Uchumi ya Ulaya na Benki ya Ujenzi na Maendeleo ya Ulaya zitatumika katika kipindi kati ya mwaka 2011 na 2013.

Pendekezo hilo linatolewa wakati viongozi wa mpito wa Misri na Tunisia wakihudhuria mkutano huo wa G8.

Elfenbeinküste Alassane Ouattara
Rais Alassane Ouattara wa Cote d'IvoirePicha: AP

Naye Rais Alassane Ouattara wa Cote d' Ivoire amesema nchi yake inahitaji kiasi cha kati ya euro bilioni 15 na 20 ili kuweza kuirejesha nchi yake katika hali ya kawaida baada ya vurugu za uchaguzi mkuu wa nchi hiyo.

Ouattara ambaye pamoja na viongozi wengine wa Afrika wanatarajiwa kuhudhuria kikao cha leo cha Dauville, amesema tayari rais Sarkozy ameahidi mkopo wa euro bilioni 2 na kumuomba rais Obama kusadia katika jambo hilo.

Mwandishi: Sudi Mnette//RTR/DPA

Mhariri:Josephat Charo

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi