1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa kijeshi wa Guine watiwa kishindo

Oumilkher Hamidou16 Oktoba 2009

Umoja wa Afrika wawataka Camara na wenzake watamke wazi hawatopigania uchaguzi

https://p.dw.com/p/K88B
Mtawala wa kijeshi wa Guine,kepteni Dadis Camara wa guinePicha: AP

Baraza la amani na usalama la umoja wa Afrika limewaonya watawala wa kijeshi wa Guinee,watachukuliwa hatua ikiwa hawatoahidi kutoshiriki katika uchaguzi mkuu ujao.Wakati huo huo Ufaransa imewataka raia wake wanaoishi Guinee,waihame nchi hiyo ya Afrika magharibi.

Kamishna wa masuala ya amani na usalama wa Umoja wa Afrika, Ramtane Lamamra, amesema wamemtaka tena kepteni Moussa Dadis Camara aahidi kimaandishi, yeye na wanachama wa baraza lake la taifa kwa ajili ya Demokrasia na maendeleo-CNDD, hawatopigania uchaguzi wa January mwakani- la sivyo,watakabiliwa na vikwazo vya Umoja wa Afrika.

"Baraza la amani na usalama limekutana na kuitaka halmashauri ya Umoja wa Afrika iandae ripoti inayofafanua vikwazo vya aina gani vitachukuliwa ikiwa CNDD hawatatilia maanani masharti yaliyotolewa."

"Mnamo muda wa saa 48 zijazo,mengi yanaweza kutokea na tunataraji kuna kitu kitakachotokea" amesema mwenyekiti wa baraza la amani na usalama la Umoja wa Afriika, bibi Nkozi Yoyo wa kutoka Nigeria.

Bibi Yoyo amezungumzia juhudi kadhaa zinazoendelea hivi sasa ikiwa ni pamoja na mkutano wa viongozi wa jumuia ya ushirikiano wa kiuchumi Afrika magharibi, ECOWAS, utakaoitishwa kesho jumamosi mjini Abuja nchini Nigeria.

"Kwa hivyo tunasubiri ili tuweze kutangaza uamuzi wetu"-amesisitiza.

Baraza la amani na usalama la Umoja wa Afrika liliwahi kutoa onyo kama hilo september 17 iliyopita na kuwapa muda wa mwezi mmoja viongozi wa kijeshi wa Guinea watoe ahadi kama hiyo. Lakini hakuna kilichotokea.

Matumizi ya nguvu na visa vyengine vya kinyama vilivyofanywa na jeshi ili kuwatawanya wafuasi wa upande wa upinzani waliokua wakidai kepteni Camara asipiganie kiti cha rais , yamegharimu maisha ya zaidi ya watu 150.

Umoja wa Afrika umeanzisha utaratibu wa kuchunguza kisa hicho na mwanasheria mkuu wa korti ya kimataifa ya uhalifu ameshaanza kuchunguza kisa hicho.

Kamishna wa Umoja wa Ulaya anaesimamia masuala ya misaada ya kiutu na maendeleo, Karel de Gucht, alisema wiki hii kepteni Moussa Dadis Camara anastahiki kushtakiwa kwa makosa ya uhalifu dhidi ya ubinaadam. Msemaji wa kamishna huyo wa Umoja wa ulaya John Clanchy anasema:

"Tumeona uhalifu ,tumeona visa vya uhalifu ambavyo mtu anaweza kusema ni vya uhalifu dhidi ya ubinaadam. Kutokana na hali hiyo,ni wazi kabisa kwamba wahusika lazima wafikishwe mahakamani."

Ufaransa imewataka raia wake 2500 wanaoishi Guinee waihame nchi hiyo kutokana na hali tete inayotawala nchini humo.

"Hakuna dalili kwamba hali itabadilika hivi karibuni"-taarifa ya wizara ya mambo ya nchi za nje imesema.

Hata hivyo, Ufaransa haijapanga kuwahamisha raia wake. Waziri wa ulinzi, Herve Morin, anazungumzia "hatua za tahadhari."Bora watu wafanye tahadhari,wachukue hatua zinazohitajika badala ya kulazimika baadae kuchukua hatua za dharura. "Amesema waziri wa ulinzi wa Ufaransa Hervé Morin.

Mwandishi Hamidou Oummilkheir/AFP/Reuters

Mhariri:Othman Miraji