1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa Sudan Kusini wanafaidika na vita

Sylvia Mwehozi13 Septemba 2016

Viongozi wa pande mbili katika mgogoro wa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan Kusini pamoja na familia zao wametajwa kufaidika kutokana na mgogoro huo.

https://p.dw.com/p/1K12T
Südsudan Rebellenführer Riek Machar in Juba
Picha: Reuters/Stringer

Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na mwigizaji wa Marekani George Clooney na wenzake, viongozi hao wamejipatia utajiri mkubwa kupitia mabenki, biashara ya silaha na makampuni ya mafuta.

Ripoti hiyo inafuatia uchunguzi uliofanywa kwa miaka miwili na shirika moja la santry ambalo Clooney ni mwanzilishi mwenza pamoja na mwanaharakati mwenzake John Prendergast na imekuja muda ambao Umoja wa Mataifa umetoa kitisho cha kuiwekea vikwazo vya silaha serikali ya Sudan Kusini.

Ripoti hiyo imetanabaisha kwamba mtandao wa waratibu wa wawezeshaji wa kimataifa uliotanuka kwanzia kwa wauza silaha nchini Ukraine hadi makampuni ya ujenzi nchini Uturuki, makampuni ya madini nchini Kenya pamoja na wawekezaji wa kichina unashiriki biashara za ubia katika kamari pamoja na sekta ya ulinzi binafsi nchini Sudan Kusini.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo rais Salva Kiir na aliyewahi kuwa makamu wake Riek Machar pamoja na majenerali wa kijeshi na familia zao wamejipatia utajiri wa nyumba na magari ya kifahari kutokana na biashara ya mafuta na ubia mwingine.

Wasemaji wa viongozi hao wawili waliwahi kukanusha kwamba wakuu hao wanamiliki mali nchini Kenya au katika mataifa mengine ya afrika kama ripoti inavyodai. Mwanaharakati John Prendergast amesema "kwa bahati mbaya , nchini Sudan Kusini, uhalifu wa vita unalipa. Viongozi hawatilii maanani vitisho vya Umoja wa Mataifa, Marekani na wengine vya kupata matokeo kutokana na tabia zao. Viongozi wa Sudan Kusni wamejifunza kwamba ubakaji, ubakaji kama silaha ya vita, kuwatumia askari watoto na mauaji makubwa havitoshi kwa wao kuchukuliwa hatua kali za uwajibikaji", alisema mwanaharakati huyo.

Askari watoto wanaotumika Sudan Kusini
Askari watoto wanaotumika Sudan KusiniPicha: picture-alliance/dpa/S.Bor

Ripoti hiyo pia imebainisha kwamba mkuu wa jeshi Paul Malong ambaye anapata dola elfu 45 kwa mwaka walau anamiliki nyumba mbili za kifahari nchini UGANDA pamoja na hekalu lingine jijini Nairobi.

Ripoti inaweka wazi kwamba wanafamilia wa viongozi wa ngazi ya juu serikalini wanamiliki hisa katika biashara mbalimbali Sudan Kusini. Familia ya rais Kiir inaelezwa kuhusika katika mfululizo wa mikataba ya manunuzi ya serikali na makampuni ya nje ya mafuta. Mtoto wa rais huyo mwenye miaka 12 anamiliki hisa asilimia 25 katika kampuni mojawapo iliyoanzishwa mwaka 2016.

Kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita viongozi hao wameshiriki matendo ya kikatili dhidi ya wananchi wake, njaa na ubakaji wakati huo wakihakikisha kwamba wanachuma rasilimali na kujitajirisha wenyewe na familia zao.

Clooney na wenzake wanataka kufanya ushawishi kwa rais Barack Obama wa Marekani pamoja na viongozi wengine wa juu kuiwekea vikwazo Sudan Kusini pamoja na kufungia mali zao zilizo nje ya nchi.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/Reuters

Mhariri: Iddi Ssessanga