1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa Syria na Urusi wakutana

MjahidA22 Julai 2013

Naibu Waziri Mkuu wa Syria Qadri Jamil yuko nchini Urusi kwa mazungumzo na waziri wa mambo ya nchi za nje juu ya namna ya kumaliza mgogoro wa Syria, uliodumu kwa zaidi ya miaka miwili sasa.

https://p.dw.com/p/19BhC
Naibu Waziri Mkuu wa Syria Qadri Jamil
Naibu Waziri Mkuu wa Syria Qadri JamilPicha: Reuters

Kulingana na afisaa mkuu wa Syria, Urusi na Syria  zitazungumzia pia uwezekano wa Urusi kutoa msaada wa kifedha kwa Syria kusaidia kuukwamua  uchumi wake uliosambaratika kutokana na vita vinavyoendelea.

Naibu waziri mkuu huyo Qadri Jamil amesema jambo hilo limezungumziwa na wanatumai kupata jibu kabla ya mwisho wa mwaka huu.

Jamil amesema kwa sasa ni mapema sana kujua ni kiwango gani cha fedha watakachopokea. Kando na hilo Syria imesema mpango wa kutatanisha wa Urusi kupeleka mfumo wa makombora  aina ya S-300 nchini humo bado inazingatiwa.

Mwanajeshi wa Syria
Mwanajeshi wa SyriaPicha: picture alliance/dpa

Wakati huo huo shirika la habari la kitaifa nchini Urusi la Interfax limesema pande zote mbili ziliamua mwezi uliopita katika mkutano uliofanyika kaskazini mwa Ireland kwamba watafanya kazi pamoja ili kuwaondoa magaidi na makundi yalio na itikadi kali nchini Syria.

Sergei Lavrov asema upinzani hauna nia ya mazungumzo

Hii leo Waziri wa Mambo ya nchi za kigeni wa Urusi Sergei Lavrov amesema upinzani bado haujaonesha nia ya kujiunga na mazungumzo hayo.

"Tunaendelea kukutana na serikali na makundi yote ya upinzani kuwashawishi wote kwamba ni muhimu kujiunga na mchakato huu wa amani haraka iwezekanavyo," Alisema Sergei Lavrov.

Waziri wa Mambo ya nchi za kigeni wa Urusi Sergei Lavrov
Waziri wa Mambo ya nchi za kigeni wa Urusi Sergei LavrovPicha: Reuters

Waziri huyo amesema pia kwa sasa idadi kubwa ya upinzani haijaonesha nia ya kujiunga na mazungumzo.

Hata hivyo ziara ya  Naibu waziri mkuu wa Syria Qadri Jamil nchini Urusi imekuja baada ya Ahmad al-Jarba, mkuu wa muungano wa upinzani nchini Syria kukutana na viongozi wa Misri na Saudia wikendi iliopita, kabla ya kuelekea Ufaransa kukutana kwa mazungumzo na rais wa nchi hiyo Francois Hollande.

Mashambulizi zaidi Syria

Huku hayo yakiarifiwa  wanaharakati wa Syria wamesema waasi 75 wameuwawa kwenye makabiliano na vikosi vya serikali saa 24 zilizopita katika kung'ang'ania udhibiti wa mji mkuu Damascus.

Idadi nyengine ya vifo ilioripotiwa na shirika la kutetea haki za binaadamu lililo na makao yake mjini London,Uingereza  inajumuisha waasi 49 waliouwawa katika shambulizi la Kaskazini Mashariki mwa mji wa Adra mapema jana asubuhi.

Ahmad Al-Jarba na Waziri wa mambo ya Kigeni wa Misri Nabil Fahmi
Ahmad Al-Jarba na Waziri wa mambo ya Kigeni wa Misri Nabil FahmiPicha: Reuters

Shirika hilo limesema vikosi vilivyotiifu kwa Rais Bashar Al Assad viliwavamia waasi hao walipokuwa wanajaribu kuingia mjini humo.

Hata hivyo shirika la habari la taifa nchini Syria SANA  liliripoti mashambulizi hayo bila kutoa idadi ya waliojeruhiwa.

Kwa sasa Shirika la Umoja wa Mataifa linakadiria watu takriban elfu 93,000 wameuwawa tangu kuanza kwa machafuko nchini Syria zaidi ya miaka miwili iliopita.

Mwandishi: Amina Abubakar/Reuters/dpa/AFP/AP

Mhariri: Yusuf Saumu