1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vita Gaza-Makombora zaid kutoka Lebanon

Eric Kalume Ponda14 Januari 2009

Kwa mara ya pili Israel imeshambuliwa kwa maroketi yaliyorushwa kutoka upande wa Lebanon ingawa hakuna majeruhi.

https://p.dw.com/p/GY6h
Wanajeshi wa Israel wakiwa oparesheni yao katika mji wa Gaza.Picha: AP


Makombora ya maroketi kutoka Kusini mwa Lebanon yalishambulia vijiji vuilivyoko eneo la kaskazini mwa Israel ingawa hakuna majeruhi walioripotiwa.Hali kadhalika Israel iliendelea na mashambulizi yake katika barabara za Mji wa Gaza na Vitongoji vyake usiku kucha huku juhudi za kimataifa zikiendelea katika kuutanzua mzozo huo



Kwa mujibu wa jeshi la Israel makombora matano ya maroketi yalishambulia vijiji vya Shebaa na Ghajar na kujibiwa vikali na jeshi la Israel ambalo lilirusha makombora sita katika muda usiozidi dakika moja.Hadi kufikia sasa hakuna kundi lolote lilodai kuhusika na shambulio hilo ambalo limetokea wiki moja baada ya shambulizi jingine la makombora kutoka ardhi ya Lebanon kutekelezwa ndani ya Israel.


Shughuli za miji iliyoko karibu na eneo la mashambulizi huko Kaskazini mwa Israel zilikwama ikiwa ni pamoja na shule kufungwa kwa kuhofia mzozo zaidi baina ya nchi hizo mbili.


Shambulio hilo limezua kumbukumbu ya vita vya mwaka wa 2006 kati ya Israel na wapiganaji wa kundi la Hezbolla waliokuwa wakiungwa mkono na Syria na Iran ambako zaidi ya watu 1,200 waliuawa.


Hata hivyo kikosi cha Umoja wa mataifa cha wanajeshi 13,000 kinachohifadhi amani katika eneo la mpakani kimeimarisha doria ili kuzuia kusambaa zaidi kwa mashambulizi hayo.


Kwa upande mwengi mwengine wanajeshi wa Israel waliendelea na mashambulio yao katika mji wa Gaza huku idadi ya Wapalestina waliouawa ikiongezeka na kufikia watu 971 na wengine zaidi ya 4,000 kujeruhiwa.

Wanajeshi hao wa Israel walikabiliana vikali na wafuasi wa chama cha Hamas katika barabara za kitongoji cha mji wa Gaza kilicho na wakaazi wengi ambako mizinga na makombora vilitawala usiku kucha. Wanajeshi hao wa Israel wanasema kuwa walishambulia vituo 60 wakati wa oparesheni hiyo ya usiku huku chama cha Hamas kikirusha makombora mawili ya maroketi yaliyoshambulia mji wa Beer Sheaba kusini mwa Israel.


Kiongozi wa shirika la msalaba mwekundu anayeongoza shughuli za misaada ya kibinadamu katika eneo hilo Jackob KellenBerger ambaye kwa mara ya kwanza aliweza kulizuru eneo lenye idadi kubwa ya watu mjini Gaza alisema kuwa hali ilivyo katika eneo hilo ni ya kusikitisha.

KellenBerber alisema..`` Naweza kusema kuwa ni hali ya kusikitisha na kuhuzunisha roho kile nilichoshuhudia katika eneo hilo la vita. Inahuzunisha kuona watu wengi waliojeruhiwa na maisha yao ni lazima yalindwe. Ni jambo lisiloweza kukubalika.Watu waliojeruhiwa hawawezi kusubiri kwa siku kadhaa au hata masaa kuokolewa na kutibiwa´´.


Katibu mkuu wa umoja wa mataifa Ban Ki Moon amewasili mjini Cairo kufanya mashauri na viongozi wa Misri, Joradn na Syria ili kutafuta suluhisho la mzozo huo. Katibu huyo mkuu alisikitishwa na hali ilivyo katika eneo la ukanda wa Gaza akisema akiitaja kuwa isiyoweza kuruhusiwa kuendelea zaidi.


Viongozi wa Israel wanasema kuwa bado wataendelea na mashambulizi yao dhidi ya Hamas huku wakisubiri matokeo ya mpango huo wa amani. Wajumbe wa Chama cha Hamas wanahudhuria mashauriano hayo na walitarajiwa kutoa mapendekezo yao kwa kuhusu vipengee vinavyohitaji kufanyiwa marekebisho.


Mpango huo wa amani unataka kusitishwa mara moja kwa mapigano katika eneo hilo, Hamas wakomeshe mtindo wa kuingiza silaha kimagendo kupitia njia za mpakani na kuwataka wanajeshi wa Israel kuondoka katika ardhi ya Gaza.


Pande hizo mbili zililikataa azimio la Umoja wa mataifa lililopitishwa wiki iliyopita liokizitaka kusitisha vita hivyo mara moja.