1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waalbania wa Kosovo washerehekea uhuru kutoka kwa Serbia

18 Februari 2008
https://p.dw.com/p/D9Ck

Walbania wa Kosovo wamejitokeza kwa wingi katika barabara za miji ya Kosovo kusherehekea uhuru wa jimbo hilo kutoka kwa Serbia.

Waziri mkuu wa Kosovo, Hashim Thaci, alitangaza rasmi uhuru wa Kosovo hapo jana baada ya bunge kupiga kura kuidhinisha tangazo hilo bungeni mjini Pristina.

Hatua hiyo imezusha hisia za hasira katika mji mkuu wa Serbia, Belgrade, ambako mamia ya vijana walifanya machafuko.

Walivunja madirisha ya majengo ya balozi za Marekani na Slovenia, nchi za magharibi zinazounga mkono uhuru wa Kosovo, kabla polisi wa kupambana na fujo kuwatawanya.

Rais wa Serbia, Boris Tadic, amesisitiza atafanya kila jitihada kuizuia Kosovo kutambuliwa na jumuiya ya kimataifa.

Rais Tadic anatarajiwa kusafiri kwenda mjini New York Marekani ambako kikao cha dharura cha baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kimeitishwa.

Wakati huo huo, mlipuko umeiharibu gari ya Umoja wa Mataifa kaskazini mwa Kosovo, saa chache baada ya Kosovo kujitangazia uhuru wake kutoka kwa Serbia.

Duru za polisi zinasema mlipuko huo umetokea baada ya grenedi kuvumishwa katika mahakama ya Umoja wa Mataifa katika kijiji cha Zubin Potoko, yapata kilomita 10 kaskazini magharibi mwa Kosovska Mitovica.