1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waandishi wa habari wanyanyaswa katika kipindi cha kampeni DRC

25 Novemba 2011

Kipindi cha kampeni ya uchaguzi mkuu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kimeghubikwa na vitendo vya unyanyasaji dhidi ya waandishi na vyombo vya utangazaji habari.

https://p.dw.com/p/13GvX
Mwandishi wa habari aliyekamatwa na polisi mjini KinshasaPicha: AP

Mashirika ya kutetea uhuru wa waandishi yamesema yanatiwa wasi wasi na ukandamizaji unaofanywa na polisi dhidi ya waandishi, na yameiomba serikali kuingilia kati ili waandishi habari nchini humo waweze kufanya kazi yao katika mazingira salama katika kipindi hiki muhimu kwa demokrasia ya nchi hiyo. Daniel Gakuba anayo maelezo zaidi.

Mnamo wiki ya mwisho ya mwezi Oktoba, mashirika mawili ya kutetea uhuru wa vyombo vya habari, "Reporters without borders" na "Journalist in Danger", yaliorodhesha visa tisa vya unyanyasaji dhidi ya waandishi habari nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Visa hivyo ni pamoja na kufungwa, kutimuliwa kwa vyombo vya habari kutoka ofisi za kazi, kunyang'anywa vifaa vya kazi na hata wakati mwingine kupigwa na polisi.

Mara nyingi unyanyasaji huo umefanywa dhidi ya waandishi habari wanaoripoti juu ya mikutano na maandamano vya wagombea wa upande wa upinzani. Katika kisa kimojawapo, mwandishi wa kituo kimoja cha Radio kiitwacho Ushirika katika wilaya ya Ritshuru alitiwa mbaroni baada ya kukutwa na picha za mtu anaegombea kiti cha ubunge kwa tiketi ya chama cha upinzani.

Logo Reporter Ohne Grenzen englisch

Lakini si polisi peke yao ambao wamewanyanyasa waandishi wa habari nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Baadhi ya wanasiasa na watu wanaowaunga mkono wamekuwa wakiwalenga waandishi ambao wanatangaza habari zisizokwenda sambamba na matakwa yao ya kisiasa. Mienendo hii ya kujichukulia sheria mkononi badala ya kutafuta nafasi ya kujieleza, ni kitu kingine ambacho wachambuzi  wanasema kinachochea hali mbaya katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi wa tarehe 28 Novemba.

Kufuatia hali hii, Reporters without Borders na Journalist in Danger, wameandika barua kwa serikali ya Kinshasa, na kueleza kuwa endapo unyanyasaji huo hautakomeshwa haraka, wananchi watanyimwa nafasi ya kuelewa habari muhimu kuhusu uchaguzi, na hawatakuwa katika nafasi ya kufanya maamuzi sahihi siku ya kupiga kura.

Mkuu wa kitengo cha Afrika kwenye shirika la Reporters without borders Pierre Ambroise, anasema kwa sasa waandishi nchi jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo wanafanya kazi katika mazingira ya vitisho.

"Kimsingi tunachotaka kuiambia serikali ni kwamba mazingira ya sasa hayawaruhusu waandishi habari kufanya kazi yao kwa uhuru," alisema Ambroise. "Wanaogopa kuwahoji wanasiasa wakihofia yale yatakayowafika iwapo kwa mfano wataongea na mwanasiasa wa upinzani. Kwa hiyo, tunataka vyombo vya serikali viheshimu waandishi, na viheshimu vyombo vya habari."

Baadhi ya visa vya fujo dhidi ya vyombo vya habari vinafanywa kama njia ya kulipizana visasi miongoni mwa wanasiasa wa kambi zinazokinzana. Kwa mfano, ofisi za kituo cha Radio na Televisheni cha Lubumbashi ziliporwa na sehemu moja kuchomwa moto, baada ya mmiliki wake Jean Claude Muyambo ambaye hapo nyuma alikuwa waziri, kutoa kauli ya kumkosoa vikali gavana wa jimbo la Moise Katumbi. Wote wawili wanamuunga mkono rais wa sasa Joseph Kabila.

Demokratische Republik Kongo Wahl Wahlen 2011 Kinshasa Medien Journalisten
Waandishi wa habari waliokamatwa baada ya kuripoti kuhusu maandamano.Picha: AP

Matangazo ya kituo kingine cha Radio na Televisheni cha Lisanga yalikatwa na serikali baada ya kupitisha tangazo la mgombea urais wa upinzani Etienne Tshisekedi, ambao ulichukuliwa kama wenye kuchochea vurugu.

Wanadiplomasia walioko Kinshasa wanasema wanaelewa hali inayowakabili waandishi habari, na kwamba huwa wakizungumza na serikali juu ya kila kisa cha unyanyasaji.

Ndio tunaelewa matatizo wanayokumbana nayo waandishi habari, na kila yanapotokea sisi huwasiliana na serikali. Ukizingatia hali ilivyo sasa, na nimekuwa nikizungumza na waangalizi wa kimataifa, inaonekana mazingira ya uandishi yanaanza kuboreka, na tunaamini itaendelea hivyo.

Radio ni tegemeo kubwa la wananchi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kuweza kujua habari za nchi yao na za dunia, na wakati wa uchaguzi kiwango cha usikivu huongezeka. Ili waweze kupata habari za kuaminika, ni lazima kuwepo na mazingira bora ya kazi kwa waandishi.

Uchaguzi wa jumatatu wiki ijayo ni wa pili kufanyika baada ya kumalizika kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyohusisha majeshi kutoka nchi sita za kikanda.

Mwandishi: Daniel Gakuba

Mhariri: Abdul-Rahman