1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waandishi wa Iran wakabiliwa na udhibiti kwenye mtandao

Adrian Fariborz / Maja Dreyer12 Novemba 2007

Kulingana na ripoti ya hivi karibuni ya shirika la “waandishi wasiojali mipaka”, Iran ni miongoni wa nchi 20 ulimwenguni zinazotoa uhuru mchache kwa vyombo vya habari. Waandishi wa habari wako hatarini kukandamizwa ikiwa hawakubali kufuata itikadi ya chama tawala. Juu ya hayo, siyo tu magazeti na vituo vya redio na televisheni, bali serikali ya kidini ya Iran inadhibiti pia yale yanaoandikwa katika mtandao wa Internet ambao ulijulikana kuwa na uhuru zaidi.

https://p.dw.com/p/CHj8
Kwenye kituo cha Internet mjini Teheran
Kwenye kituo cha Internet mjini TeheranPicha: AP

Kila siku, mhandisi Mohsen, mwenye umri wa miaka 27 hana uhakika iwapo tovuti yake kwenye mtandao wa Internet bado iko wazi. Mhandisi huyu ambaye pia ni mwandishi tangu muda wa miaka mitatu iliyopita anaandika jarida la kila siku kwenye tovuti yake. Katika lugha ya mtandao maelezo hayo yanaitwa Blogging na Bw. Mohsen ni mmoja kati ya waandishi maarufu zaidi wa Blogs nchini Iran. Zamani alikuwa mwanaharakati wa wanafunzi wa chuo kikuu na ameshawahi kufungwa gerezani.

Anadhani kuzuiliwa kwa ukurasa wake wa Internet si tokeo la pekee, bali mtandao huu umenyimwa uhuru wake. Anasema: “Tovuti yangu ya Weblog inazuiliwa kwenye vituo kadhaa vinavyotoa hudumu hizo za Internet, licha ya kwamba inataja tu kidogo juu ya masuala ya kisiasa. Hali imekuwa mbaya tangu rais Ahmadinejad alipoingia madarakani. Ninaamini kwamba tangu hapo tovuti za Interneti zinadhibitiwa na kuzuiliwa. Wanatafuta zile zinazohusu siasa na ambapo yale yanayoandikwa ni dhidi ya msimamo wa serikali. Nilipozungumzia zaidi masuala ya kisiasa, tovuti yangu ilizuiliwa kabisa.”

Tena serikali ya kidini ya Iran ina sababu kubwa ya kuwa na wasiwasi juu ya mtandao. Baada ya magazeti mengi ya mrengo wa mageuzi yalipopigwa marufuku tangu mwaka wa 2000, waandishi wengi walitumia mtandao wa Internet na kuchapisha maoni yao humo bila ya vizuizi kutoka kwa upande wa serikali. Lakini serikali pia imekodoa macho yao kwenye mtandao. Mwaka 2004 waliwakamata waandishi watatu maarufu wa mtandao wanaopinga serikali . Tovuti kadhaa zinadhibitiwa, vile vile wabunge walitoa mwito kupiga marufuku majukwaa ya vijana wanapojadili mambo yao hadharani katika mtandao kama vile Yahoo Messanger.

Tovuti hizo zinatumika sana na vijana kwa sababu wanapenda kubadilishana maoni , kama anavyoeleza mwandishi Mohsen. Hata hivyo, serikali mara kwa mara inazuia kurasa hizo ikihofia kwamba ni jukwaa la kuundwa makundi ya kisiasa. Hali ilikuwa mbaya zaidi tangu kupitishwa sheria inayosema kwamba mtu anayetoa huduma za Internet au kuendesha tovuti yake ya Blogging lazima aombe ruhusa, la sivyo adhabu ni kali.

Bw. Mohsen juu ya matokeo ya sheria hiyo: “Waandishi wa habari na vitabu wa Iran wamepunguza sana matumizi ya Internet na hawaendeshi tena kampeni za kisiasa kwa sababu hatari ni kubwa mno na unaweza kukamatwa. Wengine walioandika Blogs tayari walifungwa gerezani. Pia inabidi ujiulize ikiwa hatari hiyo kweli inalipa, kwani wale wanaosoma kwenye mtandao ni wachache.”

Juu ya hayo, waandishi wanatishiwa wasizungumze na waandishi wengine wa nchi za nje. Kulingana na shirika la “waandishi wasiojali mipaka”, waandishi wengi wa Iran hawaandiki tena maoni yao huru ili waweze kuendelea kufanya kazi. Yule anayejaribu kuzungumzia hali halisi ya kisiasa na kijamii nchini Iran atazuiliwa kama kwa mfano gazeti la meya wa zamani wa Teheren na shirika la habari la ILNA ambayo yamemlaani rais Ahmadinejad kwamba hajatimiza ahadi zake za kuboresha hali ya uchumi wa Iran.