1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waasi wa Chad waushambulia mji wa Adre unaopakana na Darfur

3 Februari 2008
https://p.dw.com/p/D1jc

Waasi nchini Chad ambao inasemekana wamesaidiwa na ndege za jeshi la Sudan, wamefanya shambulio hii leo katika mji wa Adre mashariki mwa Chad, unaopakana na jimbo la Darfur.

Afisa mkuu wa serikali ya mtaa mjini humo, Abadi Sasir, amethibitisha shambulio hilo akisema idadi kubwa ya waasi wameingia mjini humo lakini wanakabiliana nao.

Kwa mujibu wa afisa huyo waasi wa Chad wamesaidiwa na helikopta na ndege aina ya Antononov za Sudan.

Waasi na wajeshi ya serikali wanakabiliana katika mapambano ya kuudhibiti mji mkuu Ndjamena. Afisa wa serikali ya Chad amesema jeshi la nchi hiyo linaudhibiti mji wa Ndjamena.

Leo wizara ya mashauri ya kigeni ya Ufaransa imesema imewaondoa raia 514 wa kigeni kutoka Chad na kuwasafirisha hadi mjini Libreville nchini Gabon, wakiwemo wafaransa 217.

Taarifa ya wizara hiyo imesema raia wengine takriban 400 wa kigeni waliosalia mjini Ndjamena wataondolewa baadaye.

Ufaransa inapanga kuwasafirisha raia wake kutoka mjini Libreville hadi Paris hii leo.

Wakati haya ya kiarifiwa Nigeria imeliweka jeshi lake katika hali ya tahadhari huku kukiwa na hofu ya mapigano nchini Chad kuenea.