1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waasi wa FDLR wauwa watu 17 mashariki mwa Kongo

Saumu Mwasimba28 Mei 2007

Watu wanaoshukiwa kuwa waasi wa kihutu kutoka Rwanda wamewauwa kwa kuwachoma visu watu kiasi cha 17 katika eneo tete la mashariki mwa nchi ya Jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo jumapili.

https://p.dw.com/p/CHDf

Mauaji hayo ndio mabaya kabisa kutokea katika eneo hilo katika kipindi cha miaka miwili.

Afisa mmoja kwenye eneo la Kaniola kulikotokea mauji hayo, akizungumza na kituo cha Radio cha Umoja wa mataifa OKAPI alisema mashambulio hayo yamesababisha takriban watu 20 kujeruhiwa vibaya na wengi kutekwa nyara.

Gavana wa Kaniola Celestin Cibalonza akielezea juu ya mkasa huo amesema waasi wa FDLR kutoka Rwanda walikivamia kijiji cha Kaniola mwendo wa saa tano saa za Kongo huku wakiwa na visu na hapo ndipo walipoanza kuwachinja watu kiholela.

Mzee mmoja wa kijiji hicho Oscar Zihaliwa akizungumzia kile alichokiona katika tukio hilo alisema watu 15 walikufa hapo hapo baada ya kuchomwa visu baadae waasi hao waliwachinjua wengine wawili miongoni mwa watu waliowateka nyara.

Katika watu waliotekwa nyara alikuweko miongoni mwao msichana mdogo ambaye alipata nafasi na kutoroka asubuhi ya leo .Msichana huyo anasema watu 18 walitekwa nyara pamoja naye na watatu tayari wameuwawa.

Kaniola ni kijiji kilichoko yapata kilomita 50 kutoka magharibi mwa Bukavu mji mkuu wa jimbo la kivu Kusini.

Kwa muda wa miaka kadhaa sasa eneo hilo limekuwa tete na mara kwa mara kumeripotiwa uvamizi wa waasi hao wakihutu kutoka Rwanda ambao pia wanaendesha hujuma za kuwateka nyara wanakijiji.

Mbali na waasi hao pia kuna kundi lingine linalowahangaisha watu katika eneo hilo kundi hilo linalojiita Rasta na linawajumuisha wapiganaji kutoka nje na ndani ya kongo.

Mauaji hayo ya jumapili yametokea baada ya jeshi la Kongo linaloungwa mkono na kikosi cha Umoja wa Mataifa kuanzisha opresheni kali dhidi ya waasi kwenye eneo hilo mnamo mwezi wa Aprili.

Kuanzia wakati huo alau kambi moja ya waasi imeharibiwa.

Watu wa kijiji hicho wanasema mauaji ya jana ni hatua ya kulipiza kisasi iliyochukuliwa na waasi baada ya kuanzishwa opresheni dhidi yao.

Kwa sasa inasemekana waasi wa FDLR wamekimbilia sehemu ya milimani na wametoa onyo na kusema kwamba watarudi tena kuendeleza hujuma.

Idadi ya waasi hao wa kihutu wa FDLR imetajwa kuwa zaidi ya elfu kumi 10,000 na wamekuwa wakiendesha shughuli zao kwenye misitu na milimani huko mashariki mwa jamhuri ya Kongo tangu kutokea mauaji ya halaiki ya mwaka 1994 nchini Mwao Rwanda ambapo kiasi cha watutsi laki nane waliuwawa..

Serikali ya Rwanda inalaumu baadhi ya waasi wa FDLR kwa mauaji hayo.