1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waasi wa Libya wadai kudhibiti mji wa mafuta Brega

19 Julai 2011

Waasi wa Libya wanadai kuwa wamevishinda vikosi vya kiongozi wa Libya Muammar Gaddafi na wanaudhibiti mji muhimu wa mafuta Brega ulio kilomita 750 mashariki ya mji mkuu Tripoli.

https://p.dw.com/p/Raaa
Libyan rebels riding on the back of an armed pickup truck retreat during an exchange of fire with pro-Gadhafi forces along the frontline on the outskirts of Brega, Libya, Monday, April 4, 2011. (Foto:Nasser Nasser/AP/dapd)
Waasi wa Libya nje ya mji wa mafuta BregaPicha: dapd

Vikosi vya waasi wa Libya vimefanikiwa kusonga mbele na vinadai kuudhibiti mji huo wa bandari,mashariki ya Libya. Hali hiyo imekuja ikiwa ni siku tatu tu baada ya Baraza la Mpito la Taifa -TNC- lililoundwa na waasi kutambuliwa kama waakilishi halali wa umma wa Libya. Kundi maalum kuhusu Libya, lilikutana, mwishoni mwa wiki iliyopita mjini Istanbul, Uturuki ambako Marekani na nchi zingine 27 za magharibi na Kiarabu, zililitambua baraza hilo la mpito la waasi.

Lakini baadhi ya maafisa na wachambuzi huru wana shaka, iwapo ushindi wa waasi katika mji wa Brega pamoja na kutambuliwa kwa baraza hilo la mpito, kutatosha kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Libya.

In this image taken from RTP Portugal TV, filmed in Tripoli, Libya, Thursday March 17, 2011, showing Libyan leader Moammar Gadhafi, during an interview as he comments on the prospects of a United Nations resolution against Libyan government forces. The interview made available Friday March 18, was filmed Thursday before the United Nations voted to authorize the use of "all necessary measures" to protect civilians under attack by government forces in Libya. (Foto:RTP Portugal TV/AP/dapd) TV OUT - PORTUGAL OUT - Mandatory credit RTP TV
Kiongozi wa Libya, Muammar GaddafiPicha: AP/RTP TV

Kwani ionekanavyo, Kanali Gaddafi aliekuwa akivihimiza binafsi vikosi vyake katika miji kadhaa, amejizatiti katika mji mkuu Tripoli, hata ikiwa wapiganaji wa waasi hivi sasa, wanasonga mbele upande wa mashariki na magharibi. Wakati huo huo, msemaji wa serikali ya Libya, Mussa Ibrahim amesisitiza kuwa mji wa Brega, unadhibitiwa na vikosi vinavyomuunga mkono Gaddafi. Amesema kuwa waasi, walijaribu kuuteka mji huo, lakini walisukumwa nyuma na waasi 500 waliuawa katika mapigano hayo. Akaongezea:

"Huenda wakasita kupigana baada ya kuudhibiti mji wa Brega. Wanachotaka ni mafuta, lakini sisi tutautea mji huo kufa kupona."

Mji wa Brega, ni kituo muhimu cha kusafirishia mafuta hadi sehemu mbali mbali duniani. Mabomba hayo yanasafirisha mafuta kutoka bonde la Sirte lenye utajiri wa mafuta.

Waasi wa Libya, wameshindwa kumtimua madarakani Gaddafi, hata baada ya takriban miezi sita ya kupigana vikali na kusaidiwa na jumuiya ya kujihami NATO, inayotaka kuwalinda raia nchini humo. Kiongozi wa Libya Gaddafi akizidi kushinikizwa kuondoka baada ya kuwa madarakani kwa miongo minne, wajumbe wa Marekani walikuwa na mkutano wa nadra, pamoja na waakilishi wa serikali ya Libya mwishoni mwa wiki iliyopita. Afisa mmoja wa Marekani, amesema huo haukuwa mkutano wa kujadiliana bali ni kuwasilisha ujumbe kuwa, njia pekee ya kusonga mbele, ni kwa Gaddafi kuondoka madarakani.

Mwandishi: Martin,Prema/afpe,ips

Mhariri:Abdul-Rahman,Moahammed