1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waasi wa Libya wajiandaa kuingia Bani Walid

5 Septemba 2011

Vikosi vya Baraza la Mpito la waasi wa Libya vinajiandaa kuuvamia mji wa Bani Walid, huku vikitumai kuwa wafuasi wa Muammar Gaddafi watakubali kusalim amri ili kuzuia umwagaji damu.

https://p.dw.com/p/Rk27
Rebels reinforcements from Tripoli celebrate as they arrive at a checkpoint between Tarhouna and Bani Walid, Libya, Monday, Sept. 5, 2011. Negotiations over the surrender of one of Moammar Gadhafi's remaining strongholds have collapsed, and Libyan rebels were waiting for orders to launch their final attack on the besieged town of Bani Walid, a spokesman said. (Foto:Alexandre Meneghini/AP/dapd)
Vikosi vya waasi vilivyowasili kituo cha ukaguzi nje ya Bani WalidPicha: dapd

Mbali na miji ya Sebha na Sirte alikozaliwa Gaddafi, Bani Walid pia ni ngome ya Gaddafi na waasi wanaamini huenda Gaddafi na wanawe wanalindwa na wakuu wa kikabila katika eneo hilo. Waasi wamekusanyika kwa maelfu karibu na mji wa Bani Walid ulio kama kilomita 140 kusini-mashariki ya mji mkuu Tripoli, wakingojea kupewa amri ya kuuvamia mji huo. Ripoti zingine zinasema kuwa baadhi ya wafuasi wa Gaddafi wametoa silaha zao. Lakini siku chache zilizopita kulikuwepo pia ripoti kama hizo bila ya baadae ngome hiyo kudhibitiwa na waasi. Kwa vile hakuna mawasiliano, ni shida kuthibitisha ripoti hiyo kutoka ndani.

Ushindi utatangazwa baada ya kumkamata Gaddafi

Vikosi vya waasi vinadhibiti takriban maeneo yote nchini Libya na Baraza la Mpito linaunda serikali mpya. Lakini waasi hao hawawezi kutangaza ushindi mpaka watakapomkata Gaddafi na kuyadhibiti maeneo kama Bani Walid. Kwa hivyo, waasi hao wapo tayari kusubiri kwa matumaini ya kuzuia mapambano makali ya kikabila ambayo huweza yakasababisha utengano. Hata hivyo, baadhi ya waasi wameonya juu ya uwezekano wa kuuvamia mji wa Sirte na ngome zingine za Gaddafi, kwani inaaminiwa kuwa maafisa wengi mashuhuri wa serikali ya zamani wamejificha huko.

Msemaji wa vikosi vya Baraza la Mpito, Ahmed Bani, amesema wakati wa kufanya majadiliano umekaribia mwisho wake, kwa hivyo hawatokuwa na budi kutumia nguvu. Akaongezea:

"Siku tatu au nne zilizopita, kulikuwepo matumaini ya kuukomboa mji wa Bani Walid bila ya kupigana vita, lakini wao wamekataa kusalim amri."

"Kamanda Ismail al-Gitani wa kikosi cha waasi waliokusanyika kwenye kituo kimoja cha ukaguzi kiasi ya kilomita 70 kutoka mji wa Bani Walid, alisema wapiganaji hao ni sehemu ya kikosi kikubwa kinachojiandaa kuingia upande wa kaskazini wa Bani Walid. Lakini hawatoingia ndani ya mji huo bila ya kualikwa na wakaazi wa kabila la Warfala amabalo ni kabila kuu huko Bani Walid. Amesema hawataki kutumia silaha, lakini hawatojizuia iwapo watafyatuliwa risasi na wafuasi wa Gaddafi. Inaaminiwa kuwa idadi ya watu wa kabila la Warfala ni kama milioni moja, ikiwa ni takriban asilimia 17 ya umma wa Libya.

Mchakato wa demokrasia kutayarisha uchaguzi

Katika mji mkuu, Tripoli, msemaji wa Baraza la Mpito amesema, mchakato wa demokrasia utaanza kwa kutolewa tangazo la ukombozi na Baraza la Mpito kuanza kufanya matayarisho ya kuitisha uchaguzi wa bunge katika kipindi cha miezi minane. Hata hivyo, amesema bado hakuna hakika lini ukombozi utatangazwa, baada ya waasi kuidhibiti nchi nzima au baada ya kumkamata Gaddafi.

Kwa mujibu ripoti ya shirika la habari la AFP, kundi la wafuasi wa Gaddafi, akiwemo mkuu wa usalama wa ndani, Mansour Daw, limevuka mpaka na limeingia nchi jirani ya Niger, lakini watoto wa Gaddafi wala jamaa zake wa karibu hawamo katika kundi hilo.

Wakati huo huo, jumuiya ya kujihami ya NATO imeripoti kuwa imeshambulia vituo kadhaa karibu na Sirte na maeneo mengine usiku wa jana. Vikosi vya Gaddafi vinashambuliwa na NATO tangu mwezi wa Machi, baada ya operesheni hiyo ya kijeshi kuidhinishwa na Umoja wa Mataifa kwa azma ya kuwalinda raia wa Libya. Kibali cha kufanywa operesheni hiyo kinamalizika Septemba 27, kwa hivyo waasi huenda wakataka kumaliza mapigano yao kabla ya tarehe hiyo ,kwani kisiasa huenda ikawa vigumu sana kurefusha muda huo.

Mwandishi: Blaschke,Björn/zpr/-P.Martin/ape

Mharairi: Othman,Miraji