1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wajerumani watakiwa kujitathmini kwa ugaidi wa ndani

17 Novemba 2011

Wahariri wa Ujerumani wanazungumzia ugaidi uliofanywa na makundi ya mrengo wa kulia yenye siasa kali, uwezekano wa Ujerumani kuelekea moja kwa moja kwenye matumizi ya nishati jadidifu na pia mgogoro wa sarafu ya euro.

https://p.dw.com/p/13CIC
Picha ya bango la kundi la kigaidi la Ujerumani, "Nationalsozialistischer Untergrund" (NSU).
Picha ya bango la kundi la kigaidi la Ujerumani, "Nationalsozialistischer Untergrund" (NSU).Picha: dapd

Kuhusiana suala la ugaidi wa ndani, kutoka jamii ya Wajerumani wenyewe, ukiwa tofauti na ule uliozoeleka unaofanywa na wageni, hasa kutoka jamii za Kiislamu, mhariri wa gazeti la Mitteldeutsche Zeitung anazungumzia kauli ya msemaji wa masuala ya ndani wa chama cha SPD, Dieter Wiefelspütz, anayehoji picha halisi ya ugaidi hapa Ujerumani ilikuwa haijasemwa.

"Miaka kumi iliyopita, ungeliniuliza je, hapa Ujerumani tuna ugaidi, ningelijibu ndiyo, tunao magaidi wa Kiislamu. Lakini hatuna magaidi wa mrengo wa kulia, wala wa mrengo wa kushoto. Lakini kumbe jibu hilo lingelikuwa ni uongo." Amesema Wiefelspütz.

Mhariri anasema kuwa, baada ya mashambulizi ya 11 Septemba 2001, sheria na vita vyote dhidi ya ugaidi vilielekezwa kwa magaidi wa Kiislamu tu na, kwa hivyo, kosa kubwa lilifanyika. Kwa maneno ya Wiefelspütz, kosa hilo linapaswa kurekebishwa sasa.

Umeme wa jua bado ni ghali

Vioo vya kukusanyia mionzi ya jua kwa ajili ya kuzalishia umeme.
Vioo vya kukusanyia mionzi ya jua kwa ajili ya kuzalishia umeme.Picha: DW

Kufuatia uamuzi wa Ujerumani kuanza kujitenga na matumizi ya nyuklia kama chanzo kikuu cha nishati, sasa nchi inalazimika kuelekea kwenye matumizi ya vyanzo salama vya nishati, yaani nishati jadidifu. Na hilo lina gharama zake, kama mhariri wa gazeti la Rheinische Post anavyohoji.

Mhariri huyo anasema waziri wa uchumi, Phillip Rösler, anataka kuyafupisha mahitaji ya nishati ya jua hadi kufikia mwaka 2012, akitaka lazima umeme huo uwe rahisi. Kwa sasa, mtumiaji wa nishati hiyo, huenda anatumia fedha nyingi zaidi, kuliko yule mtumiaji wa vyanzo vyengine vya umeme.

Mitambo mikubwa ya kukusanyia mionzi ya jua na kuzalisha umeme, inapaswa kujengwa kwa wingi zaidi na kuzalisha angalau megawati 6,500 hadi mwishoni mwaka huu wa 2011. Lakini, mhariri anamalizia, kuifanya ndoto hiyo kuwa kweli ni rahisi kwenye maneno kuliko kwenye vitendo.

Mgogoro wa Euro waligusa Bunge la Ujerumani

Sarafu za Euro
Sarafu za EuroPicha: picture-alliance/dpa

La mgogoro wa nishati si pekee linaloikumba Ujerumani na Ulaya hivi sasa. Kuna pia mgogoro wa sarafu ya euro, ambao hata kama bado Ujerumani haijaanza kutikisika, tayari imeanza kuhisi hadi ndani ya Bunge, kwa mujibu wa mhariri wa Saarbrücker Zeitung.

Mhariri anasema kwamba sasa Rais wa Bunge, Norbert Lammert, amelazimishwa na sheria kuzikubali hotuba za wabunge wanaochukuliwa waasi dhidi ya Euro, Klaus-Peter Willsch wa CDU na Frank Schäffler wa FDP.

Mwanzoni, Lammert alikuwa amezizuia hotuba za Willsch na Schäffler, kwa hoja kwamba wasiseme kuwa ni maoni ya vyama vyao, bali yao wenyewe binafsi.

Lakini mwenyekiti wa kamati ya shughuli za CDU Bungeni, Thomas Strobl, akachukuwa hatua za kisheria, kwa hoja kuwa kutoa hotuba Bungeni, sio tu ni haki ya kila mbunge, bali ni wajibu unaoambatanishwa na uhuru wa maoni.

Vyanzo: Mitteldeutsche Zeitung/Rheinische Post/Saarbrücker Zeitung
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Josephat Charo