1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakenya wafadhaishwa na ICC

Mohamed Dahman30 Aprili 2011

Wakenya wakatishwa tamaa na mwenendo wa kesi za baada ya uchaguzi wa mwaka 2007 unaoendelea kwenye Mahakama ya Uhalifu wa Kimataifa, The Hague, kwa kutokujumuishwa uhalifu wa Kibera na Kisumu, ambao uligharimu maisha.

https://p.dw.com/p/116wG
Eneo la mabanda la Kibera, Nairobi
Eneo la mabanda la Kibera, NairobiPicha: CC/Schreibkraft

Uamuzi wa kutojumuisha uhalifu uliotendwa katika mji wa magharibi wa Kisumu na kitongoji duni cha Kibera mjini Nairobi katika kesi dhidi ya wanaodaiwa kuhusika na machafuko ya umwagaji damu kufuatia uchaguzi wa mwaka 2007 nchini Kenya, unaweza kudhoofisha juhudi za Mahkama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita kukomesha tabia ya watu kutowajibishwa kisheria kwa makosa yao katika nchi hiyo ya Afrika mashariki.

Majaji walitowa hukumu hapo mwezi wa Machi kwamba Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahkama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita ICC Luis Moreno Ocampo ameshindwa kuonyesha mauaji yaliofanywa na polisi kinyume na sheria katika mji wa magharibi wa Kisumu halikadhalika mauaji, kujeruhi kwa watu na ubakaji uliotokea katika kitongoji duni cha Kibera mjini Nairobi ni sehemu ya sera ya taifa iliowahusisha watuhumiwa watatu waliomo katika chama cha Rais Mwai Kibaki cha Umoja wa Taifa PNU.

Watuhuimiwa hao Waziri wa Fedha Uhuru Kenyatta,Mkuu wa Huduma za Umma Francis Muthaura na Kamishna wa Polisi wa zamani Mohammed Hussein Ali hivi sasa wanakabiliwa na mashtaka ya uhalifu dhidi ya ubinadamu,mauaji, kuhamisha watu kwa nguvu,ubakaji, unyanyasaji na vitendo vyengine vya kinyama kuhusiana na ghasia katika mkoa wa Bonde la Ufab.Katika kesi nyegine tafauti watuhumiwa watatu wengine pia wanakabiliwa na mashtaka ya mauaji,kuhamisha watu kwa nguvu na unyanyasaji.

Hukumu hiyo ya mwezi wa Machi inasema ushahidi wa Ocampo unatowa hoja za kutosha kuamini kwamba polisi walitumia nguvu kupindukia hususan risasi za moto dhidi ya wakaazi wa Kisumu na kusababisha vifo zaidi ya 60.Majaji pia walisema kuna ushahidi unaodokeza kwamba polisi walivamia kitongoji duni cha Kibera mara kadhaa na kwamba pia kundi la Mungiki lilifanya uhalifu kwenye kitongoji hicho.

Rais Mwai Kibaki akipiga kura ya maoni ya Katiba mpya 2010
Rais Mwai Kibaki akipiga kura ya maoni ya Katiba mpya 2010Picha: AP

Lakini kwa sababu walikuwa hawakuridhika na uhusiano uliopo kati ya uhalifu huo na sera ya taifa au watuhumiwa wenyewe binafsi majaji walitupilia mbali mashtaka hayo.

Stella Ndirangu afisa wa sheria kwa Kamisheni ya Kimataifa ya Majaji kwa Kenya amesema kushindwa kufunguliwa mashtaka kwa watuhumiwa wa uhalifu uliofanyika Kibera kutawafadhaisha wahanga wengi katika kitongoji hicho hususan kwa kuzingatia ukweli kwamba kitongoji hicho duni kilitajwa sana katika uchunguzi wa awali wa Ocampo.

Ndirangu amekaririwa akisema iwapo kutakuwa hakuna uwajibikaji juhudi za kujaribu kukomesha marudio ya vitendo hivyo zitakuwa hazina maana.

Amesema wahanga huko Kisumu watakuwa wamevunjika moyo iwapo kesi dhidi ya Kenyatta,Muthaura na Ali zitalenga tu mkoa wa Bonde la Ufa.Ameongeza kusema kwamba kwa upande wa Kisumu takriban matukio hayo yote yalikuwa yamenaswa kwenye kamera hususan pale polisi walipokuwa wakitumia nguvu.

Consolata Ngugi mwenye umri wa miaka 49 mkaazi wa kibera tokea mwaka 1994 alibakwa na wafuasi watatu wa Raila Odinga ambaye alishindwa uchaguzi wa rais na Mwai Kibaki na ambaye hivi sasa ni waziri mkuu. Amesema mchakato wa ICC ambao awali aliuunga mkono utakuwa hauna maana iwapo majaji hawatotilia maanani ushahidi juu ya uhalifu uliotendeka Kibera.

Kwa mujibu wa ombi la awali la Ocampo la kutaka kuanzisha uchunguzi serikali imekiri kwamba watu 1,220 walipoteza maisha yao nchini kote wakati wa ghasia hizo za baada ya uchaguzi ambazo zilimalizika mwishoni mwa mwezi wa Februari mwaka 2008.

Lakini Pamela Akwede mkuu wa ofisi ya haki za binadamu katika Kanisa Katoliki la Mfalme Kristo anaamini mauaji ya zaidi ya watu 1,000 yalitokea Kibera pekee.

Akwede anasema kutojumuishwa kwa Kibera katika kesi hiyo dhidi ya Kenyatta, Muthaura na Ali itakuwa sawa na telekezo la mwisho kwa wahanga ambao tayari wamedhulumiwa na wanasiasa na polisi wakati wa ghasia hizo.

Hata hivyo afisa wa ushauri wa sheria katika Mahkama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita ICC Jelena Vukasinovic amesema Ocampo anaweza kuwasilisha ushahidi mpya na mapema kabla ya kuanza kusikilizwa kwa kesi ya kuthibitisha mashtaka inayowakabili watuhumiwa wa ghasia za baada ya uchaguzi nchini Kenya hapo mwezi wa Septemba.

Mwandishi: Mohamed Dahman/IPS
Mhariri: Aboubakary Liongo