1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakimbizi wa muda mrefu waweza kushusha pumzi

Oummilkheir13 Machi 2007

Maridhiano kuhusu haki ya kuishi wageni laki moja na 80 elfu,kama watatekeleza masharti yaliyowekwa

https://p.dw.com/p/CHIE
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel
Kansela wa Ujerumani Angela MerkelPicha: AP

Wawakilishi wa vyama vikuu vya kisiasa nchini Ujerumani wamekubaliana juu ya kupatiwa kibali cha kuishi humu nchini wageni kama laki moja na 80 elfu waliokua”wakivumiliwa tuu”hapo awali.

Kila kwa mara,wanasiasa wa vyama ndugu vya CDU/CSU na wale wa SPD walikua wakibishana ,vipi na kwa masharti ya aina gani wageni kama hao wapatiwe haki ya kuishi salama humu nchini.

Mashirika ya haki za binaadam na makanisa kila kwa mara walikua wakikumbusha mazungumzoni,dhiki ya aina gani wanakumbana nayo watu kama hao, wasiojua hatima yao itakua vipi,kama watarejeshwa makwao au wataruhusiwa kusalia humu nchini.

Tangu jumatatu usiku maridhiano yamepatikana-.Mvutano wa miaka nenda miaka rudi kwa hivyo kuhusu hatima ya watu hao wanaokadiriwa kufikia laki moja na 80 elfu,umemalizika angalao kwa sasa.Watapatiwa kibali cha kuishi,ikiwa hadi mwaka 2009 watafanikiwa kupata kazi na kudhihirisha wanaweza kuzungumza kijerumani.

Zaidi ya hayo wanatakiwa wawe watu ambao hawajawahi kushtakiwa.Watu wenye kulea watoto bila ya mume au mke,wanabidi wawe wameishi angalao miaka minane nchini Ujerumani,na familia ya baba na mama na watoto wawe wameishi si chini ya miaka sita.

Maridhiano hayo yanaonyesha kua sawa nay ale yaliyowahi kufikiwa wiki kadhaa zilizopita na wasocial Democratic wa SPD na wenzao wa vyama ndugu vya CDU/CSU.

Kabla ya hapo wawakilishi wa SPD walipinga kujadiliwa upya sheria hiyo inayowaruhusu wageni kuishi humu nchini .Mwenyekiti wa chama cha SPD katika jimbo la Thüringe Christoph Matschie alisema:

“Nnahisi kila cha kujadiliwa kiimejadiliwa kuhusu haki ya kuishi.Kwa hivyo kile kilichokubaliwa kinastzahiki kutiwa njiani.”

Lakini maridhiano hayo yaliyofikiwa wiki chache zilizopita,yalikuja kutiwa ila na chama cha CSU na baadhi ya mawaziri wa mambo ya ndani wa majimbo kutoka chama cha CDU.

Maridhiano haya mepya yanajibu masharti yaliyotolewa na wanasiasa wa vyama hivyo ndugu vya CDU/CSU. Kabla ya hapo waziri mkuu wa jimbo la North Rhine Westfalia,Jürgen Rüttgers alisema:

“Nnaamini,lazma iwekwe wazi hapa,kwamba wale ambao pengine wataruhusiwa kusalia muda mrefu humu nchini,wasije wakageuka mzigo kwa bajeti za serikali.Lazma iwekwe wazi pia kwamba kila la kufanya lifanywe ili kuhakikisha kwamba watakaosalia wapatiwa kazi pia na wanakubali kufanya kazi hizo.”

Kipya ni kwamba wageni hao hivi sasa badala ya kupatiwa misaada ya fedha watakua wakipatiwa vitu tuu ili kupunguza gharama za fuko la jamii.

Serikali kuu ya Ujerumani inapanga kuidhinisha maakubaliano hayo kabla ya siku kuu ya pasaka.

Maridhiano hayo ya jumatatu iliyopita yanafungua njia ya kudurusiwa kikamilifu sheria ya uhamiaji iliyopitishwa mwaka 2005.Miongoni mwa mengineyo serikali kuu ya Ujerumani itabidi izingatie vifungu 11 vya muongozo wa Umoja wa Ulaya kuhusu sheria za uhamiaji na ruhusa ya wageni kuishi humu nchini.