1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waliofurushwa msitu wa Mau waomba serikali iwajali

29 Novemba 2011

Serikali ya Kenya inakabiliwa na changamoto ya kuulinda msitu wa Mau, na wakati huo huo kulipatia ufumbuzi tatizo la makaazi kwa watu 25 elfu waliofurushwa kutoka kwenye msitu huo mwaka 2009.

https://p.dw.com/p/13IuG
Ramani ya Kenya
Ramani ya Kenya

Watu waliofukuzwa kutoka msitu wa Mau wanaafiki juu ya umuhimu wa hatua zilizochukuliwa katika juhudi za kuhifadhi mazingira, na wakati huo huo kulalamikia maisha mabovu katika kambi walizojengewa kandoni mwa msitu huo baada ya kuondolewa katika mazingira yao ya asili.

Wengi wa watu waliofurushwa kwa nguvu kutoka katika msitu wa Mau ni kutoka jamii za Ogiek, Kipsigis na Wamasai. Mmoja wao ni Lucy Sadera kutoka jamii ya Ogiek, ambaye anasema kwao msitu huo ulikuwa mazingira pekee waliyozoea kuishi, akilinganisha umuhimu wa msitu huo kwa jamii yake na ule wa maji kwa samaki.

Wakipsigis na wamasai walihamia katika msitu huo kama walowezi kati ya mwaka 1978 na 2002, katika juhudi za serikali ya rais wa zamani Daniel Arap Moi kuwatafutia makazi mapya wahanga wa vurugu za kugombania ardhi za miaka ya 1990.

Lakini baadaye mwaka 2009, watu hao pamoja na wale ambao asili yao ni katika msitu wa Mau waliamriwa kuuhama ili kusimamisha ukataji miti ambao ulikuwa unahatarisha msitu huo. Kwa muda wa miaka miwili iliyopita wamekuwa wakiishi katika makambi ambayo hayana mahitaji muhimu kama maji na vyoo safi.

Umuhimu wa msitu wa Mau kimazingira ni dhahiri na hauna mjadala. Msitu huo ni kama tanki kubwa la gesi ya carbon na chanzo muhimu cha maji kwa Kenya. Msitu huo pia una mchango mkubwa katika kudhibiti mafuriko na mmomonyoko wa ardhi.

Kutunzwa kwa msitu wa Mau kumeongeza kiwango cha mvua ambayo ni muhimu kwa kilimo.
Kutunzwa kwa msitu wa Mau kumeongeza kiwango cha mvua ambayo ni muhimu kwa kilimo.Picha: CC/Victor Ochieng

Shirika la mazingira la umoja wa mataifa, UNEP, linasema majanga ya mafuriko na ukame ambayo yamelikumba eneo la Afrika Mashariki yametokana na kufyekwa kwa misitu. Kufyekwa kwa msitu wa Mau kumeathiri kiwango cha maji yanayosambazwa mijini na vijijini.

Hektari 20,000 za msitu huo ziliokolewa kufuatia kufukuzwa kwa watu. Ingawa huo ulikuwa ushindi kwa mazingira, kwa jamii ya Ogiek ilikuwa dawa chungu sana kumeza. Jamii hiyo ndogo ambayo inakadiriwa kuwa na watu ishirini elfu tu, imeishi katika msitu huo tangu enzi za mababu zao.

Msitu wa Mau ni mali ya umma, lakini baadhi ya vigogo katika siasa waligawiwa vipande vikubwa vya ardhi ndani ya msitu huo kama zawadi kwa kuiunga mkono serikali iliyokuwepo madarakani. Watu hao lakini hawana hati za kimiliki ardhi hiyo. Hata hivyo haijulikani hatua gani zitachukuliwa dhidi yao.

Eliud Bonosos kutoka jamii ya Ogiek anasema wanakasirishwa na uamuzi wa serikali kuwaondoa katika mazingira yao asilia, licha ya kuwepo kwa ushahidi kuwa uharibifu wa msitu huo ulianza tu baada ya walowezi kuingia.

''Msitu huu ni ardhi ya mababu zetu, tunajua namna ya kuishi bila kuharibu mazingira yetu. Hawawezi kujiuliza kwa nini uharibifu ulianza katika muongo mmoja uliopita''? Anauliza Bonosos.

Mtu mwingine, Kantau Nkuruna kutoka shirika la Community Forest anasema katika kipindi cha miaka 20 iliyopita, msitu wa Mau umepoteza asilimia 25 ya eneo lake kutokana na makazi haramu, ukataji holela wa miti, na kuchoma mkaa.

Tangu kuanzishwa kwa harakati za kuutunza msitu wa Mau mwaka jana, kiwango cha mvua kinaonekana kuongezeka. Hilo ni muhimu kwani msitu huo ni chanzo cha mito inayotiririka katika maziwa muhimu kama vile Naivasha, Victoria, Turkana na Natron.

Msitu ni chanzo muhimu cha mito
Msitu ni chanzo muhimu cha mitoPicha: DW / Kateri Jochum

Kuangamia kwake kungekuwa na athari zinazovuka mipaka ya Kenya. Waziri wa ardhi wa Kenya James Orengo anasema makosa yalifanywa siku za nyuma lakini sasa yanakosolewa.

Changamoto inayobakia na yenye kuamsha hisia ni hatima ya jamii zilizofurushwa kutoka msitu huo, kwa vile baadhi ya wanasiasa kutoka jamii hizo wanadai kufukuzwa kwao ilikuwa njia iliyotumiwa na serikali kuwaadhibu watu kwa sababu ya mitazamo yao kisiasa.

Mwandishi: Daniel Gakuba/IPS

Mhariri:Othman Miraji