1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wapalestina 12 wauwawa katika Ukanda wa Gaza

Josephat Charo27 Juni 2007

Wapalestina 12 wameuwawa na wengine zaidi ya 40 kujeruhiwa leo wakati wanajeshi wa Israel walipoyavamia maeneo ya kaskazini na kusini mwa Ukanda wa Gaza. Wakati huo huo waziri wa mashauri ya kigeni wa Ujeruamni, Fank Walter Steinmeier, ameonya juu ya mgawanyiko wa kudumu baina ya Waspalestina.

https://p.dw.com/p/CHC2
Kifaru cha jeshi la Israel katika Ukanda wa Gaza
Kifaru cha jeshi la Israel katika Ukanda wa GazaPicha: AP

Israel imetuma wanajeshi wake wa ardhini katika maeneo ya kaskazini na kusini mwa Ukanda wa Gaza hivyo kusababisha mapiganao makali kuzuka tangu kundi la Hamas lilipolidhibiti eneo hilo wiki mbili zilizopita. Duru za hospitali zinasema wanamgambo 12 wa kipalestina na kijana mmoja wa umri wa miaka 12 wameuwa kwenye mapambano hayo.

Duru za hospitali zinasema watu wengine takriban 40 wamejeruhiwa kwenye mapigano hayo yaliyozuka wakati wanajeshi wa Israel walipovuka mpaka na kuikaribia miji wa Khan Younis na Gaza. Mapiganao makali yamekuwa yakiendelea katika kitongoji cha mji wa Gaza cha Sheja´eya karibu na kivuko cha Karni katika mpaka na Israel ambako watu 10 waliuwawa. Aghalabu wanamgambo wawili wameuwawa kwenye ufyatulianaji wa risasi huko Khan Younis.

Msemaji wa jeshi la Israel amesema wanajeshi walikuwa katika operesheni dhidi ya vitisho vya ugaidi katika eneo hilo, lakini hakutoa maelezo zaidi. Wapalestina walioshuhudia wanasema miongoni mwa waliouwawa ni kamanda wa kundi la Islamic Jihad, Radi Fanouna, na kijana wa miaka 12 mpitanjia wakati helikopta ya Israel ilipoilenga gari yake kwa kombora. Lakini jeshi la Israel limekanusha madai hayo likisema halikuhusika na kifo cha kamanda huyo.

Mpalestina wa 13 mwanachama wa kikosi cha kundi la Hamas, ameuwawa alipokuwa akijaribu kutengua bomu lililopatikana kwenye uwanja wa usalama katika mji wa Khan Younis kusini mwa Ukanda wa Gaza.

Mapiganao ya leo yametokea kufuatia hatua ya pande nne zinazoudhamini mpango wa amani ya Mashariki ya Kati kudokeza azma yao ya kutaka kumteua waziri mkuu wa Uingereza aliyeondoka, Tony Blair, kuwa mjumbe wake maamulu kuushughulikia mgogoro wa Mashariki ya Kati. Waziri mkuu wa Ireland, Bertie Ahern, amethibitisha kuwa Tony Blair yuko tayari kuchukua wadhifa huo.

Hata hivyo tangazo rasmi lilitarajiwa kutolewa na Marekani, Umoja wa Ulaya, Urusi na Umoja wa Mataifa hii leo. Hapo awali Urusi na baadhi ya nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya zilisita kuhusu uteuzi wa bwana Blair katika kama mjumbe wa Mashariki ya Kati.

Wakati huo huo, rais wa mamlaka ya Palestina, Mahmoud Abbas, amewafuta kazi maafisa zaidi wa usalama kufuatia kushindwa kwa vikosi vyake na wapiganaji wa Hamas huko Gaza. Kiongozi wa kikosi cha kumlinda rais Abbas, jenerali Misbah al Bheisi, naibu wake kanali Ziyad Judeh, na kamanda wa kikosi cha usalama, kanali Manar Mohammed, wametimuliwa kwa kuyakimbia makao makuu ya mamlaka ya Palestina mjini Gaza bila kupigana.

Wakati haya yakiarifiwa, waziri wa mashauri ya kigeni wa Ujerumani, Frank Walter Steinmeier, ameonya juu ya mgawanyiko wa kudumu baina ya Wapalestina. Steinmeier amesema hatua ya kundi la Hamas kulidhibiti eneo la Ukanda wa Gaza haipaswi kuruhusiwa iyagawe maeneo ya Wapalestina.

Steinmeier ameongeza kusema hakuna chaguo lengine kwa serikali ya dharura iliyoundwa na rais wa mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas katika Ukingo wa Magharibi wa mto Jordan. Amesisitiza umuhimu wa kuboresha hali ya kibinadamu ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza ili kuzuia hali hiyo kuendelea kuzorota.