1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WASHINGTON: Bush aitaka Iran iwaachilie mateka wa Uingereza

1 Aprili 2007
https://p.dw.com/p/CCDR

Rais George W Bush wa Marekani ameitaka Iran iwaachilie huru wanamaji wa Uingereza waliokamatwa siku tisa zilizopita. Aidha rais Bush amewaeleza mabaharia saba na wanajeshi wanane wa jeshi la maji la Uingereza kama mateka na kusema tabia ya Iran kuendelea kuwazuilia haisameheki.

Rais wa Iran, Mahmoud Ahmadinejad, amejibu matamshi ya rais Bush kwa kuzieleza dola kuu duniani kuwa kaidi kwa kushindwa kuomba msamaha juu ya kile anachokiita hatua ya mabaharia wa Uingereza kuingia katika eneo la bahari lililo himaya ya Iran.

Kufikia sasa Iran haijakubali kuwaachilia wanamaji hao inayowazuilia katika eneo la siri, licha ya kukabiliwa na shinikizo kubwa.

Ripoti ya awali kwamba balozi wa Iran nchini Urusi, Gholamreza Ansari, alitoa matamshi kwenye runinga moja ya Urusi kwamba wanamaji hao huenda wakashtakiwa, imepingwa na manadiplomasia huyo. Ansari amesema alieleweka vibaya.