1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroMamlaka ya Palestina

UN, Saudia zaonya kuhusu operesheni ya Israel huko Rafah

10 Februari 2024

Umoja wa Mataifa, Saudi Arabia na Ujerumani zaonya kuhusu operesheni ya jeshi la Israel inayopangwa kuendeshwa huko Rafah na kusema itasababisha "janga la kibinaadamu".

https://p.dw.com/p/4cFo2
Ukanda wa Gaza | Miili ya watu waliouawa huko Rafah
Raia wa Palestina wakikagua miili ya watu waliouawa kufuatia mashambulizi ya Israel huko Rafah ambako karibu watu 25 waliuliwa usiku wa kuamkia Jumamosi: 10.02.2024Picha: Ibraheem Abu Mustafa/REUTERS

Saudi Arabia, imesema siku ya Jumamosi kwamba operesheni ya jeshi la Israel inayopangwa kuendeshwa huko Rafah  itasababisha "janga la kibinadamu" huku ikilitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuingilia kati.   

Taarifa iliyotolewa na wizara ya mambo ya nje ya ufalme huo, imeeleza wazi kuwa Saudia inapinga na kulaani vikali hatua hiyo, huku ukionya juu ya kile walichokiita "athari za mashambulizi ya kuvizia" huko Rafah na kitendo cha kuwahamisha kwa mabavu raia wa Palestina.

Soma pia: Israel yapanga kufanya operesheni ya ardhini mjini Rafah

Taarifa hiyo ya Saudia imesisitiza: "Ukiukwaji huu unaondelea wa sheria za kimataifa za kibinadamu, unaonyesha ulazima wa kuitisha mkutano wa dharura wa Baraza la Usalama ili kuizuia Israel kusababisha maafa ya kibinadamu."

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu akiongoza kikao cha Baraza la Mawaziri mjini Tel-Aviv:24.12.2023Picha: Ohad Zwigenberg/AP/dpa/picture alliance

Siku ya Ijumaa, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu aliamuru jeshi lake kujiandaa kuwahamisha raia kutoka Rafah kabla ya operesheni iliyopangwa ya ardhini dhidi ya kundi Hamas katika  mji huo wa kusini mwa Ukanda wa Gaza wanakoishi Wapalestina zaidi ya milioni moja waliokimbia makazi yao.

Wasiwasi wa Umoja wa Mataifa na Ujerumani

Umoja wa Mataifa umesema una wasiwasi mkubwa kuhusu mustakabali wa maisha ya raia wa mji wa Rafah. Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa antonio Guterres, Stephane Dujarric amesema kile kilicho dhahiri ni kwamba watu hao wanatakiwa kulindwa na kuongeza kuwa wasingependa kuona idadi kubwa ya watu wakilazimishwa kuyahama makaazi yao.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani | Annalena Baerbock
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Annalena BaerbockPicha: Ebrahim Noroozi/AP Photo/picture alliance

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Annalena Baerbock ameonya kwamba operesheni hiyo ya Israel katika mji wa mpakani wa Gaza wa Rafah itasababisha "janga la kibinadamu."

Soma pia: UN yahofia usalama wa raia walioko Rafah

Watawala wa Hamas wameonya siku ya Jumamosi kwamba operesheni hiyo ya jeshi la Israel huko Rafah inaweza kusababisha vifo vya "makumi ya maelfu" ya watu katika mji huo ambao umekuwa kimbilio la mwisho kwa Wapalestina waliokimbia makazi yao kufuatia vita vinavyoendelea katika Ukanda wa Gaza.

Kulingana na Wizara ya Afya inayodhibitiwa na Hamas, takriban watu 25 wameuawa wakati mashambulizi ya anga ya Israel katika mji wa Rafah usiku wa kuamkia Jumamosi. Hadi sasa idadi ya vifo huko Gaza imefikia watu 28,064.

(Vyanzo: ap/afp/dpa/reuters)