1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Uchumi

Watafiti: Uchumi unaimarika lakini lipo ombwe kwa Wamarekani

12 Desemba 2023

Rais wa Marekani Joe Biden anaelekea kwenye uchaguzi wa mwaka ujao huku akikabiliwa na changamoto ambapo uchumi wa Marekani umeimarika lakini watu wa nchi hiyo bado wanakabiliwa na matatizo lukuki.

https://p.dw.com/p/4a5RG
Uchumi | Rais wa Marekani Joe Biden
Rais wa Marekani Joe BidenPicha: Evan Vucci/AP Photo/picture alliance

Watafiti na wataalam wa masuala ya kiuchumi wanasema hakujawahi kuwepo pengo kubwa kama hili la sasa kati ya ustawi wa uchumi na mtazamo wa umma. 

Tofauti hiyo iliyopo kati ya kukua kwa uchumi wa Marekani na hali halisi wanayokabiliana nayo raia wa nchi hiyo,  huenda ikaamua iwapo rais Joe Biden mgombea wa chama cha Democrats atashinda muhula wa pili madarakani katika uchaguzi wa mwaka 2024.

Chama cha Republican kinatumia hali hiyo ya kutoridhika kwa raia ili kumburuza Biden, wakati Ikulu ya White House ikipata mafanikio kidogo pale inapojaribu kutetea maendeleo ya kiuchumi.

Mtafiti wa chama cha Democrats Celinda Lake, ambaye amewahi kufanya kazi na rais Biden anaelezea hatari ya hali hiyo kwamba mambo yanaelekea kuwa mazuri kiuchumi lakini watu wana dhana kuwa hali itazidi kuwa mbaya zaidi.

Soma pia:Marekani : Makubaliano ya kusitisha mapigano kwa saa 72 yakubaliwa Mashariki mwa Kongo

Lake anasema wapiga kura hawahitaji kuona mfumuko wa bei ukipungua, lakini wanahitaji kuona bei za bidhaa zikipingua, jambo linaloweza kuwa na matokeo ya moja kwa moja katika matumizi yao.

Bila shaka, uchumi wa Marekani uko imara. Takwimu zimeonyesha kuwa nafasi mpya za ajira zipatazo 199,000 zimeanzishwa mwezi Novemba huku kiwango cha ukosefu wa ajira kikishuka hadi asilimia 3.7.

Mfumuko wa bei umepungua mwaka huu kutoka asilimia 9.1 hadi 3.2% bila kusababisha mdororo wa uchumi, jambo ambalo limesifiwa na baadhi ya wachumi.

Wamarekani hawaridhishwi na hali ya uchumi

Kulingana na tafiti ya maoni ya Chuo Kikuu cha Michigan, bado idadi kubwa ya raia wa Marekani wanaonekana kutoridhishwa na hali ya kiuchumi nchini mwao. Hisia kama hizo zimeonekana kuongezeka kwa kasi zaidi miongoni mwa wanachama wa Republicans kuliko wale wa Democrats.

Uongozi | Rais wa Marekani Joe Biden
Rais wa Marekani Joe BidenPicha: Anna Moneymaker/Getty Images

Joanne Hsu, mchumi na mkurugenzi wa utafiti huo, amesema watumiaji wamekuwa na hisia ya kwamba Marekani haijarejea katika hali ya kawaida kiuchumi tangu lilipozuka janga la UVIKO-19.

Lakini Jared Bernstein, mwenyekiti wa Baraza la Washauri wa Uchumi katika Ikulu ya White House anasisitiza kuwa uchumi imara ni jambo la muhimu na anatoa hoja kwamba kadri uchumi unavyoendelea kuimarika, ndivyo watu wengi zaidi watatambua faida yake na hisia zao zitabadilika na kuwa njema zaidi. Anasema hilo linahitaji muda zaidi.

Ikulu ya White House imefanya mabadiliko matatu makubwa katika namna ya kuwasilisha ujumbe wake kwa raia, kwa matumaini ya kujenga imani katika uongozi  wa Biden hasa kuhusu suala la uchumi.

Soma pia:Utafiti: Hotuba hasi za kisiasa zaongezeka Marekani

Katika msimu huu wa kiangazi Biden alianza kutilia maanani hotuba zake kwa kutumia kauli mbiu "Bidenomics" ili kuelezea sera zake, neno ambalo WaRepublican wamekuwa wakilitumia kushambulia Biden.

Aidha maafisa wa Ikulu ya White House wamekuwa wakinadi bidhaa ambazo bei zake zimeshuka, kwa mfano kupungua kwa bei ya batamzinga wakati wa sherehe za "ThanksGiving" na pia mayai.

Biden amesisitiza mara kwa mara kwamba alipunguza gharama za dawa ya kutibu kisukari kwa waliopo kwenye mfumo wa afya wa "Medicare", huku maafisa wengine wakijadili ni jinsi bei ya mafuta ya petroli imeshuka maradufu.

Aidha, hivi karibuniBiden ameanza kuyatupia lawama makampuni kuhusu mfumuko  wa bei na kusema walitumia fursa hiyo ya kupandisha bei za bidhaa ili kujiongezea faida.

Lakini hoja hiyo inatiliwa shaka na wachumi walio wengi, lakini ujumbe unaokusudiwa kwa wapiga kura wa Marekani ni kwamba Biden anawapambania dhidi ya wale anaosema wanachochea mfumuko wa bei.

Mikopo na madhila yake